LICHA ya kuwapo kwa shutuma
mbalimbali zinazopinga mpango wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kuanzisha kikundi cha kujihami cha Red Brigade kitakachotoa ulinzi kwa viongozi
wao, imebainika kuwa msajili wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa alitoa
baraka za kuanzishwa kwake.
Tanzania Daima imeona
nakala ya barua ya mwaka 2005 kutoka katika ofisi ya Tendwa, ikionyesha kubariki
jambo hilo ambalo katika siku za hivi karibuni limezua gumzo kubwa na
kusababisha Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, kuhojiwa na polisi kuhusiana
na kauli zake.
Uchunguzi wa kina
uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kuwa Desemba 30, 2004 ofisi ya msajili wa
vyama siasa ilimwandikia Katibu Mkuu wa CHADEMA barua yenye kumbukumbu Na.
RPP/CHADEMA/72/29 ikitaka ufafanuzi baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari
kuwa chama hicho kinataka kuanzisha kikundi cha kujihami (Red
Brigade).
“Kulingana na Ibara ya 9
(2) (c) ya Sheria Na. 5 ya Vyama vya Siasa 1992, ibara ya 147 na 148 ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria ya Jeshi la Polisi, kuanzishwa kwa
kikundi hicho ni kinyume cha sheria hizo,” imeeleza sehemu ya barua
hiyo.
Barua hiyo ambayo Tanzania
Daima inayo iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa vyama vya
siasa, inaeleza kuwa kuvunjwa kwa sheria hizo kutasababisha CHADEMA
kufutwa.
CHADEMA baada ya kupata
barua hiyo, Januari 6 mwaka 2005 iliijibu kuwa kikundi kinachozungumziwa ni
walinzi wa ndani ya chama, vijana wa kike na wa kiume, wanachama wa CHADEMA,
watu wasio na silaha, chini ya usimamizi wa kurugenzi ya ulinzi na usalama ya
chama hicho.
“Kikundi kinachokusudiwa
kuundwa ni kutokana na Katiba ya CHADEMA ambayo inaruhusu uundwaji wa Kurugenzi
ya Ulinzi na Usalama chini ya Katiba ya CHADEMA, kifungu cha 7.6.4 (h),”
inaeleza barua ya CHADEMA yenye kumbukumbu Na. C/HQ/ADM/64 iliyosainiwa na Suzan
Kiwanga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CHADEMA.
Chama hicho kiliilaumu
serikali kwa vitisho ilivyotoa vya kutaka kukifuta endapo kingeendelea na
kusudio la kuanzisha kikundi hicho.
Hata hivyo, baada ya
ufafanuzi huo, Januari 11 mwaka 2005, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa,
ilipopata majibu hayo ya CHADEMA, ilieleza kuwa kwa madhumuni yaliyoelezwa na
chama hicho inakubaliana na malengo ya kuanzisha kikundi cha ulinzi kwa ajili ya
usalama wa ndani ya chama.
“Ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa, kwa madhumuni mliyoyatoa kwenye barua yenu C/HQ/ADM/62 inakubaliana
na maelezo yenu ya kuanzishwa kwa kikundi cha ulinzi kwa ajili ya usalama wa
ndani ya chama ingawa Katiba ya CHADEMA haijatoa ufafanuzi huo, vinginevyo
tunawatakia kila la heri kwenye matayarisho ya uundwaji wa kikundi hicho,”
ilisema barua ya msajili wa vyama vya siasa nchini.
Barua hiyo yenye kumbukumbu
Na. RPP/CHADEMA/72/32 iliyosainiwa na Hilda Lugembe kwa niaba ya msajili wa
vyama vya siasa nchini, pia iliwatakia kila la heri CHADEMA kwenye matayarisho
ya uundwaji wa kikundi hicho.
Nakala za majibu ya Ofisi
ya Tendwa kwa CHADEMA zilipelekwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wakati huo, Omar
Mapuri, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, aliyekuwa anashughulikia Habari na
Siasa, Muhammed Seif Khatib; Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu; Inspekta
Jenerali wa Polisi na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai.
CHADEMA waibua
mjadala
Julai 9 mwaka huu akisoma
maazimio ya Kamati Kuu ya CHADEMA mbele ya vyombo vya habari, Mwenyekiti wa
chama hicho, Mbowe alitangaza mpango wa kuboresha vikundi vya mafunzo ya
kujilinda.
Baada ya kauli hiyo watu
mbalimbali akiwemo Rais Jakaya Kikwete, walijitokeza kuupinga mpango huo kwa
madai kuwa utasababisha uvunjivu wa amani na utulivu vilivyodumu kwa muda mrefu
hivi sasa.
Ofisi ya msajili wa vyama
vya siasa pia alimwandikia barua Katibu Mkuu wa CHADEMA yenye kumbukumbu Na.
112/123/16A/3 kukitaka chama hicho kuacha kutekeleza mpango huo kwani kufanya
hivyo ni kukiuka sheria za nchi ikiwamo sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992
hali inayoonyesha kujikanganya kwa ofisi hiyo kwani awali ilisharuhusu kitu
hicho.
Barua hiyo kutoka ofisi ya
msajili inaongeza kuwa; “Kifungu cha 9(2) (c) cha sheria ya vyama vya siasa
kinakataza chama cha siasa kuruhusu kutumika, kushabikia au kutumia nguvu na
vurugu ili kufikia malengo yake ya kisiasa.”
Kwa mujibu wa barua hiyo
iliyosainiwa na Sisty L. Nyahoza kwa niaba ya Msajili wa Vyama vya Siasa, madai
ya CHADEMA kusema kuwa “Chama Cha Mapinduzi (CCM) wana kambi za mafunzo ya
kupambana isiwe kisingizio cha vyama vingine vya siasa kuvunja sheria ya vyama
vya siasa.”
Msajili pia kupitia barua
hiyo amesema “kama CCM wanakiuka sheria, ni jukumu la CHADEMA, kila chama na
kila Mtanzania kutoa taarifa na ikiwezekana na ushahidi katika taasisi husika
ikiwamo ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ili suala hili lishughulikiwe
kisheria.”
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa
CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa katika majibu yake aliifahamisha Ofisi ya Msajili
kuwa matumizi ya nguvu ikiwamo silaha kwa ajili ya ulinzi wa maisha au mali
yameruhusiwa na sheria ya jinai kanuni ya adhabu sura ya 16 ya sheria ya
Tanzania.
“Nimeshangazwa sana na
kauli yako kwamba vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa vinapaswa kuwa na
wanachama wasiokuwa na mafunzo ya kijeshi au ukakamavu kama ilivyo kwa walinzi
wa majumbani, kauli hii inadhihirisha ufahamu wako mdogo wa mambo haya. Kwanza
walinzi wa majumbani na maofisini wanaoajiriwa na utitiri wa kampuni binafsi za
ulinzi zilizosajiliwa nchini kwetu hupatiwa mafunzo ya ulinzi na ukakamavu na
wengine hupatiwa silaha za moto,” alisema Slaa.
Alisema kauli hiyo ya
msajili wa vyama vya siasa kwamba jukumu la vikundi vya ulinzi si kupambana na
wahalifu au watu wanaotaka kuwadhuru, ni hatari sana kwani inawapotosha wananchi
wasitumie haki yao ya kujilinda wanaposhambuliwa au kudhuriwa na wahalifu wa
kisiasa.
“Barua yako inatutishia
kwamba endapo tutatekeleza mpango wetu wa mafunzo kwa kikundi chetu cha ulinzi
utakuwa si uamuzi wa busara kwa uhai wa chama chetu.
“Kwa maneno mengine endapo
tutatekeleza haki yetu ya kujilinda kama tunavyoruhusiwa na sheria za nchi yetu,
kama tulivyoeleza katika barua hii, utatumia mamlaka yako kumaliza uhai wetu
kama chama cha siasa kwa kufuta usajili. Hatutaki kuamini kwamba na wewe pia
unatumiwa na CCM kukandamiza na kutoa vitisho kwa chama kingine kwa manufaa
yake,” alisema Dk. Slaa

No comments:
Post a Comment