UTANGULIZI
Aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu wa chama cha Demokrasia na
Maendelea(CHADEMA), Dkt. Kitila Mkumbo akiongea na vyombo vya habari leo
1. Katika kikao cha Kamati Kuu ya CHADEMA kilichofanyika tarehe 20-22
Novemba 2013, pamoja na mambo mengine, kulijadiliwa waraka wa siri
unaojulikana kama Mkakati wa Mabadiliko 2013. Waraka huu ulilenga
kujenga hoja ya kufanya mabadiliko ya uongozi na kuanisha mikakati ya
ushindi kwa mgombea mlengwa katika uchaguzi mkuu ndani ya CHADEMA.
Nilikiri kuwa nilikuwa naufahamu waraka huu, na kwamba nilishiriki
kuuandaa na kuuhariri, na kwamba mimi ni mmoja wa wanachama wanaoamini
kwamba kuna haja ya kubadilisha uongozi wa juu wa chama katika uchaguzi
ujao ndani ya chama.
2. Katika mjadala, maudhui ya waraka huu
yalionekana kwa wajumbe kwamba yalikuwa na mapungufu na yalikiuka
misingi na kanuni zilizoanishwa katika Katiba ya Chama. Kwa kuwa katika
chama cha siasa hoja za watu wengi ndizo hupewa uzito, na kwa kuwa
dhamira na nia yangu ndani ya chama hiki imekuwa ni kusukuma mabadiliko
ambayo watanzania wanayatazamia nje ya mfumo wa sasa wa utawala,
nilikiri makosa yangu na kuwaomba msamaha wajumbe wa Kamati Kuu na
viongozi wakuu wa chama, na kueleza kwamba nilikuwa tayari kujiuzulu na
kubaki kuwa mwanachama wa kawaida. Wajumbe walikataa kukubali ombi langu
la kujizulu bali walipitisha azimio la kunivua mimi na Mhe. Zitto
Zuberi Kabwe nafasi zetu za uongozi. Nilipokea kwa unyenyekevu adhabu ya
kuvuliwa nafasi zote za mamlaka nilizokuwa nazo ndani ya chama hiki na
kueleza kuwa nitaendelea kutoa mchango wangu kama mwanachama wa kawaida
hadi hapo chama kitakapoona ninafaa kukitumikia katika nafasi yeyote.
3. Kufuatia mkutano wa waandishi wa habari siku ya Ijumaa tarehe 22
Novemba 2013 ambapo, pamoja na mambo mengine, ilielezwa na viongozi wa
CHADEMA kwamba mimi na wenzangu (Samson Mwigamba na Zitto Kabwe)
tumehujumu chama na tumefanya uhaini kwa kuandaa mkakati wa ushindi kwa
mgombea tunayemtaka, ningependa nieleza mambo yafuatayo:
a.
Siamini hata kidogo kwamba kugombea nafasi yeyote iliyo wazi ndani ya
chama cha siasa ni uhaini na hujuma. Msingi namba moja wa CHADEMA ni
demokrasia na hakuna namna ya kudhihirisha mapenzi kwa demokrasia zaidi
ya kuruhusu ushindani katika nafasi za uongozi na hasa uongozi wa juu
kabisa. Hiki kinachoitwa uhaini ni wasiwasi wa siasa za ushindani katika
chama chetu.
b. Sijawahi na sitarajii kushiriki vitendo
vyovyote vya kuhujumu chama changu cha CHADEMA na harakati za mabadiliko
hapa nchini. Chama hiki kiliniamini katika nafasi nyingi nyeti sana na
kama mie ningekuwa mhujumu nilikuwa na fursa nzuri za kufanya uhujumu
huo. Nimeshiriki kuandaa ilani ya chama ya 2010-2015, kuratibu kampeni
za mwaka 2010 nikiwa makamu mwenyekiti wa kampeni chini ya Profesa
Baregu na nilishiriki kutengeneza na kusimamia utaratibu mzuri wa kupata
wabunge wa viti maalumu katika chama chetu. Zote hizi ni nafasi nyeti
mno ambazo kamwe huwezi kumkabidhi mtu ambaye ni ‘mhaini’ na ‘mhujumu’.
Nilishiriki katika shughuli za chama kwa kiwango ambacho
nilijisababishia matatizo makubwa katika familia yangu na kazini, lakini
sijawahi kutetereka na sijaterereka. Nilifanya yote haya kwa mapenzi
yangu ya dhati na imani yangu kwa CHADEMA kwamba ndicho chama
kinachostahili kuongoza harakati za mabadiliko hapa nchini kwa sasa.
c. Nasikitika kwamba nimesababisha usumbufu kwa viongozi wangu wa
CHADEMA kutokana na dhamira yangu ya kutaka mabadiliko ya uongozi ndani
ya chama chetu kwa njia halali za kidemokrasia. Nilifanya hivi kwa imani
niliyo nayo kwa misingi ambayo CHADEMA inasimamia, ikiwemo demokrasia,
na imani yangu kwamba chama hiki kinahitaji kufanya mabadiliko makubwa
katika uongozi wa juu wa chama, ikiwa ni maandalizi muhimu kuelekea
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015. Nasisitiza tena kwamba siamini hata kidogo
kwamba matamanio ya mabadiliko ya uongozi ndani ya chama, na kuandaa
mikakati ya kufikia matamanio hayo kwa njia za kidemokrasia ni uhaini.
d. Tunaweza kujifunza kutokana na historia. Siasa za ushindani ndani ya
vyama katika nchi hii sio kitu kigeni. Enzi za TAA na kabla TANU
haijazaliwa wanachama walikuwa wanagawana nafasi za uongozi mezani.
Lakini mwaka TANU ilipozaliwa (mwaka 1954) kulikuwa na uchaguzi mkali
sana kwa nafasi ya uenyekiti. Mwalimu Nyerere alimshinda Mzee Skyes kwa
kura chache sana. Rais Obama wa Marekani alianza mkakati wa kushinda
uteuzi wa kugombea nafasi ya urais kupitia chama chake cha Democrat
mapema kabisa mwaka 2006 kupitia waraka maalumu wa siri ulioainisha
mikakati yake. Waraka huu uliandaliwa na watu wanne tu bila yeye
mwenyewe kujua. Waandaji wa mkakati huu walikuja kumshirikisha baadaye
mwaka 2007 na kumshawishi yeye ajitokeze kugombea dhidi ya Hillary
Clinton aliyekuwa anachukuliwa kama mrithi halali wa kiti cha urais.
Yaliyobaki ni historia. Hivi ndivyo ambavyo siasa za ushindani ndani ya
vyama hatimaye huzaa wagombea na viongozi imara katika nchi.
e. Zitto Zuberi Kabwe hajafukuzwa kwa sababu ya waraka huu kwa sababu
yeye hakuhusika kwa namna yoyote kuuandaa, ingawa alikuwa ni mlengwa
mkuu. Yeye amefukuzwa kwa sababu ambazo yeye atazieleza na ambazo
viongozi wa CHADEMA hawakuzieleza katika mkutano na waandishi wa habari.
f. Napenda ijulikane kwamba sikuomba kujiuzulu kwa sababu ya
kuogopa aibu ya kufukuzwa. Niliomba kujiuzulu kwa sababu nilitambua
kwamba wenzangu katika Kamati Kuu walikuwa hawana imani nami tena, na ni
uungwana kujiuzulu mkifika mahala hamuaminiani. Nilitambua vilevile
kwamba, kwa mujibu wa Katiba yetu, Kamati Kuu ilikuwa haina uwezo wa
kunivua nafasi yangu moja kwa moja.
Kwa mujibu wa Katiba ya
CHADEMA, Sura ya Sita, Ibara ya 6.3.6 (b), inasomeka hivi “Kiongozi
aliyeteuliwa na vikao vya uongozi ataweza kusimamishwa au kuachishwa
uongozi na kikao kilichomteua”. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu na ni
kikao hiki pekee chenye uwezo wa kunivua nafasi niliyokuwa nayo.
Ninaamini wajumbe wa Kamati Kuu walipitiwa katika hili kwa sababu
siamini kwamba hawajui takwa hili la kikatiba ukizingatia kwamba ndani
yake kuna wajumbe waliobobea kabisa katika tasnia ya sheria.
4. Hiki kilichotokea ndani ya chama sio kitu kibaya. Vyama vingi imara
hupitia katika migogoro na misukosuko kama hii na zaidi. Naamini
tutavuka na tutakuwa imara zaidi. Muhimu ni kwamba ni lazima tuaminiane.
Katika kuaminiana sio lazima tufanane kimawazo na kimtazamo kwa sababu
hili ni jambo lisilowezekana kibinadamu na zaidi katika siasa.
5. Ninapohitimisha, ninawasihi wanachama wa CHADEMA na wapenzi wa
mabadiliko popote walipo wapiganie kwa dhati MISINGI mama ya CHADEMA
ikiwemo demokrasia ndani ya chama. Hakuna namna ambavyo chama chochote
kinaweza kushawishi umma kwamba kitapigania demokrasia katika nchi
wakati kinayahainisha mapambano ya kidemokrasia ndani ya chama chenyewe.
Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu
demokrasia na ni usaliti kwa misingi mama ya chama ambayo ni uhuru wa
kweli na mabadiliko ya kweli. Hisia za usaliti na umamluki zilitumika
enzi za ukomunisti katika kunyamazisha wapinzani ndani ya vyama vya
siasa na katika nchi. Zilikuwa ni njia haramu zilizozoeleka ambazo
hatimaye zilizaa udikteta wa kutisha katika mataifa ya kikomunisti.
Tusikubali utamaduni wa kuhisiana usaliti na umamluki ukaota mizizi
katika chama chetu na katika nchi kwa sababu utaua demokrasia na mfumo
wa vyama vingi utakuwa hauna maana tena.
6. Nitafuata taratibu
zote za chama kama zilivyoelekezwa na Kamati Kuu na kwa mujibu wa
katiba yetu, na nitashiriki kikamilifu katika kutuliza hali ya kisiasa
ndani ya chama ili kuhakikisha kwamba tunabaki imara, na CHADEMA
inaendelea kuwa tumaini la watanzania.
Mungu ibariki Tanzania.
Dkt. Kitila Mkumbo
Dar es Salaam
Jumapili, 24 Novemba 2013.
No comments:
Post a Comment