Edwin Bliss C

Success does not mean the absence of failure; it means the attainment of ultimate objectves. It means winning the war, not every battle.

Kufanikiwa hakumaanishi kushinda kila jambo; kunamaanisha kufikia malengo. Kunamaanisha kushinda vita na sio kila pambano.

Tuesday, January 22, 2013

WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WAMTAKA KIKWETE KULIFUNGULIA GAZETI LA MWANAHALISI



NDUGU waandishi wa habari,

Kwa mara nyingine tena, leo hii MISA - TAN, tukiwa pamoja na wanamtandao wa watetezi wa haki za binadamu, chini ya mwamvuli wa Tanzania Human Rights Defenders (THRD-Coalition), kusanyiko la asasi zaidi ya 60 za kiraia, tumewaiteni hapa kuwaomba mtufikishie ujumbe wetu huu maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.

Ujumbe ambao tunataka kuufikisha kwa Rais Kikwete, si mwingine, bali ni ombi mahususi la kutaka aingilie kati na kuamuru kufunguliwa kwa gazeti la uchunguzi la kila wiki la MwanaHALISI.

Tumewaita kutaka mtusaidie kufikisha ujumbe huo maalum kwa kwa mkuu wa nchi kwa sababu tano zifuatazo:

Kwanza, ninyi ni mashahidi wa jinsi serikali ya Rais Kikwete inavyojigamba kuwa inasimamia misingi ya utawala bora nchini. Mtakuwa mmesikia na; au mmeona jinsi viongozi waliopo madarakani wanavyohubiri kuwa wanasimamia utawala bora, wakati matendo wanayoyafanya yanakwenda kinyume na dhana hiyo.

Hivyo basi, siyo busara wala afya kwa Rais Kikwete kuongoza serikali inayosema inasimamia utawala wa sheria, demokrsia na misingi ya utawala bora, huku watendaji wake wakitenda kinyume na kile anachokihubiri.

Pili, leo ni siku ya 175 tangu waziri mwenye dhamana na masuala ya habari atumie “sheria katili ya Magazeti ya Mwaka 1976Newspaper Act 1976 – ambayo serikali hailazimiki kumueleza mchapishaji mapema wala kueleza sababu za uamuzi wake wa kufungia chombo chochote cha habari; kwa kutumia kifungu hicho, akaamuru kulifungia “kwa muda usiojulikana,” gazeti la kila wiki la MwanaHALISI.

Huo ndio ufedhuli wa sheria ambayo Tume ya Jaji Nyalali ilisema, zaidi ya miaka 20 iliyopita, kwamba ama ifutwe kabisa au ifanyiwe marekebisho makubwa.

Kipindi hiki cha siku 175 ni sawa na miezi mitano na siku 24 au miezi sita kasoro siku sita. Pamoja na wito uliotolewa mara kadhaa na taasisi huru za vyombo vya habari, asasi za kiraia; wafanyakazi na wasomaji wa MwanaHALISI, kutaka kufunguliwa kwa gazeti hilo, waziri wa habari amekuwa kimya na amegoma kusikiliza kilio hiki.

Tangu kutangazwa kwa uamuzi huo, tarehe 30 Julai 2012, serikali imekuwa kimya; huku wafanyakazi wa MwanaHALISI wakiwa hawajui hatima yao.

Ndugu waandishi wa habari,
Neno “kwa muda usiojulikana” lililoelezwa na waziri wa habari wakati wa kufungia MwanaHALISI, maana yake ni mpaka waziri atakapofurahi. Atakapojisikia. Atakapoombwa na atakaposhinikizwa vya kutosha na wapigania uhuru wa habari.

Tatu, tunamtaka Rais Kikwete aingilie kati suala hilo kwa sababu, Waziri Mkuu Mizengo Kayanza Peter Painda, aliliambia Bunge mjini Dodoma, tarehe 16 Agosti 2012, kwamba “suala la kufungiwa kwa MwanaHALISI liko kwenye mamlaka ya juu ya nchi”

Waziri Mkuu alisema, “Kama kuna mtu yoyote asiyeridhika na uamuzi wa kulifungia gazeti la MwanaHALISI akate rufaa katika mamlaka ya juu.” Waziri Mkuu hakusema, MwanaHALISI waende mahakamani. Alitaja mamlaka ya juu, na kwamba mamlaka ya juu ya Waziri Mkuu hayawezi kuwa waziri wa habari. Mamlaka ya juu ya Waziri Mkuu ni Rais.

Nne, tunamtaka Rais alifungulie MwanaHALISI kwa sababu, Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Said Mwema, ameuthibitishia ulimwengu kuwa tukio la kutekwa, kuteswa na kisha kutelekezwa akiwa nusu mfu, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dkt. Steven Ulimboka, kulikofanywa usiku wa tarehe 26 Juni 2012 na baadaye kupatikana katika msitu wa Mabwepande, wilayani Kinondoni, jijini Dar es Salaam asubuhi yake, “Ni siri ya Taifa.”

Kwa nini tunahusisha kauli ya IGP Mwema juu ya kutekwa kwa Dkt. Ulimboka na kufungiwa kwa MwanaHALISI?

Sababu ni moja: Kwamba ninyi mnajua kuwa kufungiwa kwa MwanaHALISI kulitokana na gazeti hilo kufumua taarifa ambazo zilikuwa na mvuto wa kipekee kuhusiana na kutekwa kwa Dkt. Ulimboka ambaye aliwaongoza madaktari nchini katika kudai maslahi bora, vitendea kazi pamoja na mazingira bora ya kazi.

Ni gazeti hili lililokuwa likitoa taarifa za ndani za uchunguzi ambazo zingeweza kuisaidia serikali kujiondoa katika tuhuma za kupanga njama ovu za kumteka raia wake ili kumdhuru. Kufungiwa kwa MwanaHALISI kulitokana na kuanika ushahidi mwanana usiotiliwa chembe ya mashaka kuhusiana na wanaotuhumiwa kuhusika na utekaji huo.

Aidha, kufungiwa kwa MwanaHALISI kulifuatia hatua ya gazeti kumtaja Bw. Ramadhani Ighondu, kuwa ndiye aliyehusika na kupanga njama za kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka. Hili limethibitishwa na hata Dkt. Ulimboka mwenyewe wakati alipokuwa katika hospitali ya Muhimbili na baadaye aliporejea nchini kutoka kwenye matibabu nchini Afrika Kusini.

Kauli ya IGP Mwema, inathibitisha kuwa Ramadhan Ighondu alihusika katika kumteka na kumtesa Dkt. Ulimboka; madai ya Dkt. Ulimboka kuwa Ramadhani Ighondu ni ofisa wa Ikulu, yanaonekana kuwa ni ya kweli.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano, inatambua haki ya kuishi. Hivyo basi, watetezi wa haki za binadamu wanasema kitendo cha kufungia gazeti kwa kufichua wanaohatarisha uhai wa raia, hakiwezi kufumbiwa macho kwa kisingizio kuwa mhusika ni mfanyakazi wa Ikulu.

Tano, suala hili la kulifungia gazeti la MwanaHALISI, ni miongoni mwa mambo ambayo yameanza kuipaka matope serikali ya Rais Kikwete mbele ya macho ya wanaopenda demokrasia na kuheshimu uhuru wa kujieleza ulimwenguni.

Taarifa ambazo MISA Tan na washirika wake wamezipata zinaonyesha kuwa suala la MwanaHALISI; kutekwa na kuteswa kwa Dkt. Ulimboka na kuuawa kikatili kwa bomu kwa mwandishi wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten, Daudi Mwangosi na mengine mengi, yameanza kuhojiwa na taasisi za kimataifa, ikiwamo Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Ulimwenguni (UNHCHR), pamoja na nchi wahisani, jambo ambalo linaipaka doa Tanzania.

Tayari baadhi ya wafadhiri na wadau wa maendeleo wa Tanzani wameanza kuhoji kama kweli mambo haya ya kufungia vyombo vya habari yanatokea Tanzania – nchi ambayo inajitapa kuheshimu na kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora?

Si hivyo tu, hata baadhi ya viongozi wa kidini wa ndani ya nchi, wameanza kutilia mashaka mwenendo huu wa serikali. Kiongozi mmoja wa kidini ametueleza kuwa hivi sasa wamekumbwa na woga wa kutoa mahubiri ya kuikosoa serikali katika nyumba zao za ibada.

Anasema wameanza kuhofia usalama wao na uhuru wao wa kutoa maoni kwa kuwa “serikali inayofungia gazeti linalosema ukweli, basi haitashindwa kufungia viongozi wa kidini wanaokosoa mwenendo wa serikali.”

Ndugu waandishi wa habari,
Tunataka Rais Kikwete afahamu kuwa hili si jambo jema hata kidogo kwa mustakabali mwema wa taifa letu. Ndiyo maana tunamuomba kuingilia kati kufungulia gazeti hili.

Tunasema hivyo kwa sababu miongoni mwa viashiria vikuu vya udikteta popote duniani ni pamoja na kuminya uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutoa maoni na kuwatishia wanaharakati wanaodai haki za raia.

Hakuna taifa linaloweza kutaka liheshimiwe katika jamii ya kimataifa wakati taifa hilo linaendeleza ukandamizaji wa haki nchini mwake. Haliheshimu uhuru wa kupata habari na kutoa maoni. Halitekelezi kwa vitendo mikataba ya kimataifa iliyoridhia.

Ndugu waandishi wa habari,
Tunasikia kuwa Rais Kikwete ni msikivu. Hili tumelisikia mara nyingi likisemwa na wanasiasa wenzake katika chama na serikali. Ametajwa mara kadhaa ndani ya Bunge tukufu la Jamhuri ya Muungano kuwa “Rais wetu ni msikivu.” Kama kauli hizo ni za kweli, basi tunataka asikie kilio hiki. Alifungulie MwanaHALISI mara moja na bila masharti.

Tunataka afanye hivyo leo. Siyo kesho au keshokutwa. Tunasisitiza leo kwa sababu, wananchi wanataka kuona nchi yao inaendeshwa kidemokrasia kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment