1: UTANGULIZI.
Sina budi kumshukuru sana mwenyenzi
Mungu kwa kunitendea mema na zaidi ya yote kunipa uhai na afya hadi
sasa.Wanasema “shukuruni katika yote” na mimi nalazimika kushukuru kwa yale yote
niliyofunuliwa na kuwa sehemu ya ushuhuda wangu katika maisha niliyobakiza hapa
duniani.
Namshukuru Mungu muweza wa yote kwa
kunirejesha tena uraiani na kwa kuniunganisha na familia yangu,mke na
watoto,wazazi ,ndugu,majirani na marafiki,viongozi wenzangu na wanachama wa
chama kikubwa CHADEMA na zaidi ya yote watanzania walio wazalendo wanaoipenda na
kuipigania nchi yao.
Ninapojikuta huru nje ya milango ya
mninga uliowekewa makufuli makubwa,madirisha yenye nondo,ukuta uliowekewa waya
wenye miiba mikali na ulinzi wa maaskari wanaonichunga saa 24,inanikumbusha
wimbo mmoja wa mchakamchaka uliokuwa ukiimbwa gerezani kila siku saa 11:00
alfajiri tunapoamshwa uliokuwa na maneno;
“Kama raia!kama raia!kama raia!kama
raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa baba
na mama kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa
ndugu na rafiki kama raia!
Kama raia…….”
Ni kweli kabisa na wala si hadithi
kuwa ‘jela ni MBAYA, jela ni MATESO!’
Lakini zaidi ya hilo, kwangu mimi
nimeyaona pia maisha ya gerezani ni mahala pa mafunzo ya kuijua jamii, kuyajua
maisha, kuyaelewa mambo, kuifahamu nchi n.k.
Nimekubaliana mia kwa mia na maneno
ya mwenyekiti wetu wa CHADEMA-Taifa Freeman Mbowe(MB) aliponitembelea gerezani
Segerea na kuniambia; “hupaswi kulia na kujuta sana;now you are going to be a PRISON GRADUATE, uhitimu ambao kila
mwanasiasa na mpigania haki mahiri duniani ameupitia.” Kipindi cha siku 92 nilichokaa ndani
nikianzia polisi kituo cha kati, gereza la Keko na kisha kumalizia Segerea
kimenipa uzoefu na ufahamu usio wa kawaida.
Ipo tofauti kubwa baina ya idara za
polisi na magereza,jambo ambalo lilikuwa nje ya ufahamu wangu kabla.Nina uhakika
magereza wakipewa kazi ya kuwasaka walipua mabomu ,watesaji,wapiga risasi
mapadri watawakamata.
Nilipata bahati ya kuitwa na kufanya
mazungumzo na wakuu wa magereza ya Keko na Segerea .Lakini pia, nilitembelewa na
viongozi wakuu wengi wa jeshi la magereza nchini akiwemo kamishena mkuu
Minja.Wakuu hawa wana weledi mkubwa wa kumpa mtu somo la ‘ushauri
nasaha’(counselling).Wanakufutia fikra zote za uraiani (nyumbani,mitaani na
ofisini) na kukurejesha mahala pa maisha yako mapya ya gerezani na kukujuza
taratibu na kanuni unazopaswa kuzifuata na kuzitii.
Madaktari na manesi waliweza
kuangalia kwa karibu sana afya yangu kiasi cha kulidhibiti kwa kiasi kikubwa
tatizo langu la sukari ambalo limekuwa likinisumbua kwa miaka 14
sasa.
2: KESI YA
UGAIDI.
Ni kesi ambayo imenifikisha hatua au
ngazi nyingine ya maisha yangu kama mwanasiasa.Naamini wahusika walipoamua
kuifungua bila shaka mwelekeo ulikuwa uleule ambao niliusoma nikiwa chuo kikuu
na ninaousoma katika maandiko mbalimbali kuhusu historia za wanaharakati na
wapigania haki,uhuru na ukombozi waliopita na tulio nao au tunaowasikia hivi
sasa duniani;wakina Nelson Mandela, Martin Luther King Jr n.k. Wakiwa katika harakati za kuitafuta haki
walifunguliwa kesi na wengine kufungwa jela kwa tuhuma za ugaidi,uhaini na kula
njama.
Nilikubaliana na dhana ya kimtazamo
iliyopo au waliyonayo viongozi /watawala
wote wadhalimu duniani kuwa watu wote wanaojitokeza kupambana au
kukabiliana na mfumo kandamizi bila
woga, watu wote hao kwao ni magaidi,mahaini,wala njama au wasaliti.
Ni kipindi kifupi kilikuwa kimepita
tangu timu teule maalumu ilipokuwa imemaliza kikao cha kujitathmini kama CHADEMA
(RETREAT) kuona tumetoka wapi, tuko wapi na kwa mfumo upi na mazingira yapi
ilikuyafikia malengo tuliyonayo.Nakumbuka miongoni mwa mambo niliyoyasema ni
pamoja na nini tutarajie baada ya CHADEMA kuonekana na kuthibitika kwa watawala
kwamba imekua,imeimarika na imejipanga vyema kiasi cha kuwatia hofu watawala
(CCM) kwamba karibu wanaondolewa madarakani.
Niliwaambia washiriki wenzangu kwamba
wajiandae kukamatwa na polisi mara kwa mara,kutiwa ndani,kufunguliwa kesi nyingi
zisizo za kweli,kubambikiziwa kesi,kuchafuliwa mbele ya jamii,kutishiwa maisha,
kupigwa, kuuwawa, kudhohofishwa kiuchumi n.k.
Nikasema, pindi tukiona hayo
yamekamata kasi kila pembe ya nchi tujue CCM tumeanza kuwashika pabaya na
ushindi utakuwa umekaribia.
Nilishauri tujipange kisawasawa
kimbinu na kimkakati kukabiliana na mambo hayo kwa sababu ni lazima
yatokee.Namshukuru Mungu yameanzia kwangu na kama nilivyomwambia mwenyekiti
Mbowe aliponitembelea gerezani nilimwambia
nimekipokea kikombe hiki na yaliyonitokea tusiyashangae bali yawe
changamoto na gia ya kutusukuma kwenda mbele kwa kasi kubwa zaidi.Ni kukanyaga
mafuta zaidi mpaka kieleweke na hiyo ndiyo itakuwa faraja yangu mimi na wengine
watakaofungwa magerezani.
Tuhuma za ugaidi nilizobambikiziwa
zilinirejesha nyuma mwaka 2002 nilipokuwa bungeni kama mbunge wa jimbo la Bukoba
mjini (CUF) nikiiongoza kambi rasmi ya upinzani iliyokuwa ikijumuisha wabunge
wote wa vyama vya upinzani TLP,NCCR-Mageuzi,CHADEMA,UDP na CUF.Muswada wa sheria hiyo ya ugaidi ukiwa
ndio umeletwa bungeni kujadiliwa,niliongoza kambi yangu ambayo miongoni mwao
walikuwamo Mh. Mbowe wakati huo akiwa waziri wangu kivuli wa biashara na viwanda
na Dr. Willibroad Slaa akiwa waziri kivuli wa katiba na sheria kuupinga na
kuukataa muswada huo kwa nguvu zote. Sababu mojawapo ya kuupinga ikiwa ni
mahudhui na malengo ya muswada huo kutoeleweka na kuwa wazi na kwamba ulilenga
zaidi matakwa ya kijasusi ya nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani na kwa
hapa kwetu tulitamka bayana kwamba serikali ya CCM ililenga kuitumia sheria hiyo
kuvidhibiti vyama vya upinzani.
Hilo ndilo limetokea sasa na
likaanzia kwangu.
Ukiachia mbali msongo mkali wa mawazo
niliokuwa nao nikiwa gerezani juu ya ugonjwa wa baba yangu mzazi mzee Elias
Lwakatare aliyeletwa Dar Es Salaam kwa ajili ya matibabu,athari za mke wangu
kuathirika kimasomo huko chuo kikuu Mzumbe aliko,mshtuko kwa watoto wangu
shuleni na ugumu wa karo zao za shule,kuwaweka roho juu kaka,dada na ndugu
zangu,kuvurugika kwa kazi za chama ofisini kwangu na mkoani kwangu Kagera
n.k,binafsi nililiona tukio hilo kama nafasi nyingine kwa chama chetu kujitambua
na kujipima udhaifu tulionao,nguvu tulizonazo na fursa tulizonazo wakati
tunapoelekea kuikamata dola.Niliisoma makala mojawapo ya Mwanakijiji katika
toleo mojawapo la Tanzania Daima,niliipenda sana na niliguswa. Makala hiyo
ilikuwa ikituasa CHADEMA kujitathmini. Ukweli wenyewe ni kama makala hiyo ya
Mwanakijiji sisi kama CHADEMA ilituvua nguo na kutuacha uchi.
Kwanza tuhuma ya ugaidi niliiona kama
kombora la mwisho la serikali ya CCM kukamilisha mkakati wao wa kuichimbia
CHADEMA kaburi ambayo siku zote huwa ni ya pembe nne na katika kuichimba na
kuifukia kawaida koleo lenye umbo la ‘U’ mbele na mpini wake
hutumika.
“U” ya kwanza yenye kutubamkikizia
tuhuma za ufamilia,Ukabila,Uchagga,Ukaskazini alikuwa amebebeshwa mwenyekiti
Mbowe zikashindwa.
“U” ya pili yenye kuzoa tuhuma za
Udini,Ukatoliki,Upadri alibebeshwa katibu mkuu Dr.Slaa nazo zikakwama CHADEMA
ikapenya.
“U” ya tatu yenye kulenga
Uchonganishi,Umbea,Ufitinishaji na Usongombingo, CCM wakalenga kumbebesha Naibu
katibu mkuu kijana Zitto Kabwe lakini naye akawashtukia akawaumbua na kuwabwaga.
Zitto ameendelea kuhimiza mshikamano mkubwa ndani ya chama na kuwaacha wapambe
nuksi hoi.
“U” ya mwisho yenye kubeba
Ugaidi,Uuaji,Utekaji iliyolenga kukifuta kabisa chama vitabuni na kuwasweka viongozi gerezani, kabambikiziwa Wilfred
Lwakatare Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama CHADEMA.Mungu mkubwa nayo hiyo
mahakama kuu yenye baadhi ya majaji weledi wa sheria na wasiokubali mizengwe
wameifutilia mbali.Hakika CHADEMA haizuiliki na kwa hakika lililobaki ni
kulitumia koleo hilohilo na “U” hizo kuwafukia CCM humohumo kwenye
kaburi walilojichimbia wenyewe. ‘Mchimba kaburi huingia yeye
mwenyewe.’
Nashukuru CHADEMA hivi sasa
imejipanga kama taasisi makini inayoongozwa na kusimamiwa kitaasisi na wala si
kwa utashi wa mtu binafsi au kundi fulani la watu bali vikao vya kikatiba.
Mshikamano wa pamoja na fikra zinazotuelekeza kulenga paala pamoja
tulikodhamiria, hivi sasa ndiyo silaha kubwa na nusuru yetu kichama. Kama
CHADEMA inavyoamini ; “TUNAANZA NA
MUNGU, TUNAENDELEA NA MUNGU NA TUNAMALIZA NA MUNGU.”
I AM REALLY PROUD OF BEING IN CHADEMA
FAMILY!!!
3: HALI NA TASWIRA YA POLISI MAGEREZA
NA VYOMBO VYA KUSIMAMIA HAKI NA USALAMA.
Wakati nikihojiwa na jopo la maofisa
wa makao makuu ya polisi la akina Mhigulu wakati huo akiwa Kaimu DCI na wenzake
akina Obadia,Jonas,Simon Pasua,Beneth Kipasuka,Nyombi na wengineo baadhi yao
niliwapa ujumbe wamfikishie ‘college mate’ wangu (IGP Said Mwema ) Chuo kikuu
cha Dar es Salaam kuwa naziona jitihada na mbio zao za kuwatafuta hao watu
wanaoitwa magaidi,wateka madaktari na waaandishi,wapiga risasi mapadri n.k mbio
zao haziwezi kufaulu kutokana na namna wanavyoliendesha zoezi.
Niliwaambia ;wakati wao wako ndani ya
land rover 109 kilomita arobaini nyuma yetu sisi tunaokimbizwa na kutuhumiwa kuhusu ugaidi na
kupanga njama za kudhuru watu, wahusika halisi wa mambo hayo wako na Range Rover
kilomita arobaini mbele yetu. Je,ni mwaka gani watawafikia na kuwaweka mbaroni
hao jamaa?Hivi, kikosi cha IGP Mwema ambacho tumeelezwa ni maalum na kina
makachero waliobobea kushindwa kurejesha mrejesho wa maana hadi sasa kwa angalau
hata tukio moja, hivi watanzania hatushtuki
tu? JK haushtuki ? Anyway,tuendelee kuwapa masurufu na kuwatengea mafungu
tutaona! Sijui kama walinielewa au kumfikishia IGP Mwema huo ujumbe wangu.Na kwa
kuwa asiyetaka kujua maana haambiwi maana basi tuendelee mambo ni kanyaga
twende!
Wakili wangu Kichehere niliyekuwa naye katika
mahojiano wakati nikihojiwa kituo cha kati alijaribu kuwapa changamoto japo
chache za kupanua akili zao kuhusu huo unaoitwa ugaidi dhidi yangu na ‘ka-cd’
kao walikokachota kwenye mtandao wa “You Tube” (kama walivyotueleza) na
kutuonyesha pale kwenye mahojiano. Hawakutaka kumsikiliza wala kumuelewa juu ya
kasoro zilizojidhihirisha moja kwa moja . Hata pale alipowashauri kuwaita na
kuwahoji baadhi ya watu muhimu walioonekana kuhitajika ili kuondoa walakini usio
na sababu tangu mwanzo wa zoezi, hawakutaka kuuchukua ushauri huo. Wakaona
waendelee kukimbia na hako ‘ka 109’ kao. Mimi naamini upo wakati ambapo
mshtukiwa wa tukio linalochunguzwa aliye mzalendo na nchi yake anaweza kuwa
msaada wa kuinusuru nchi yake anayoipenda endapo anapewa nafasi ya kutoa
ushirikiano kwa njia za kuheshimiana kiutu .
Anyway,sijui mwisho wa mambo yote haya maana
bado tuko safarini na bado nina kesi moja ya kujibu ya njama ya kumdhuru Denis
Msacky kwa sumu (kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama kuu ya jaji Kaduri).Sitaki
kuingilia mwenendo wa kesi hiyo na nikajiibulia mengine.Lakini kaka yangu IGP
Mwema endelea kutangaza bingo la mamilioni labda
utafaulu,Inshallah!!
Ukiacha kesi yangu hiyo ya kutuhumiwa
ugaidi, lakini kukaa kwangu pale polisi central (kituo cha kati),gerezani,keko
na Segerea kumenithibitishia vituko na mambo chungu nzima niliyokuwa nikiyasikia
nikiwa uraiani na kufikiria ni ya uongo.
Vitendo vya watu kubambikiwa kesi
viko njenje na wenyewe kwa lugha zao wanaita; “kumpa mtu kichwa! kumpiga mtu
armed robbery! kumpeleka mtu mapumziko!n.k” Nafikiri watu wanaofanya vitendo
hivi wanahitaji kufanyiwa ‘concelling…’ ( kupewa ushauri nasaha) kwani sio
vitendo vya kiutu.
Hivi huu ni utamaduni gani na taifa
tunalipeleka wapi? Hivi kweli inaingia akilini wakati mchezo kama huo ukiendelea
na watu kibao kubambikiziwa kesi kwa ‘kupewa vichwa’ wakati huohuo mh.JK yuko
‘busy’ kuwatunuku watu nishani za utumishi uliotukuka? ‘This is a typical
shame!!’ Sijui kama usalama wa Taifa wapo. Hivi wanafanya kazi gani kama
hawamsaidii mheshimiwa Rais kumjuza kinachoendelea? Au ni ugonjwa uleule
mchanganyiko wa ‘sisiemhosis’. Naanza kukubaliana na usemi wa mtu mmoja
niliyeongea naye gerezani Segerea aliyesema vyombo vya kulinda usalama huenda ni
vya kulinda usalama wa viongozi walaji,wahujumi wa nchi,mafisadi na mfumo
aliouita ; “chukua chako mapema.” Na ni vyombo vyenye weledi mkubwa wa kuchora
michoro ya fitina,uongo,wizi,hujuma,kusambaratisha vyama vya upinzani kuiba kura kutisha watu kutengeneza kesi
bandia,kuandaa mashahidi feki n.k. Matokeo yake watu ambao leo hii wamejaa na
kurundikwa magerezani na mahabusu za polisi,asilimia kubwa wanakuwa hawana hatia
wahalifu wakubwa wako nje wakiendelea kula nchi! Asilimia kubwa ya kesi
zinazopelekwa mahakamani ni feki na ni za kuwachosha mahakimu na majaji bila
sababu kwani kesi hizo huishia kufutwa.
Mrundikano mkubwa magerezani wa wafungwa na
mahabusu unasababisha hata huduma ziwe mbovu. Wapo wafungwa hawana sare za
gereza wanavaa kitu kinachoitwa ‘nusu mlingoti’, kauka nikuvae, sare
zilizochanika kiasi cha kutia aibu.Na kwa kuwa hata sera za uendeshaji magereza
nyingi ni zilezile za ‘vichwa vya ki-CCM’ (chama dhaifu,wabunge dhaifu na
serikali dhaifu) hakuna akili inayoweza kubuni namna ya kuitumia kiufanisi nguvu
kazi kubwa iliyojaa magerezani. Ndani ya gereza kuna kila aina ya fani na vipaji
lakini vimelala tu. Kama vile CCM, hawazai na hawana watoto nyumbani, huwezi
kuamini watoto lukuki waliorundikwa Segerea bila utaratibu mzuri wa kimalezi na
kimakuzi hata kama baadhi yao ni wakorofi na wahalifu. Tutake, tusitake hawa ni
taifa la leo na la kesho.Hawa ni nguvu kazi yetu ya nchi ,hawa wanahitaji
kukunjwa wangali wabichi.
Watoto hawa ambao wengine ni wa umri
wa miaka kumi wenye kesi za kuiba embe tano,kuiba simu, kudokoa pochi zenye elfu
30,000/=n.k,wamo gerezani wakinyweshwa uji asubuhi,ugali wa dona na mchuzi
mwingi wenye maharage thelathini kwenye bakuli na muda unaobaki kuutumia
kufundishana ngumi,kupiga ‘vice’, na mengine mengi. Kuna kitu kipya ambacho
kimebuniwa na uongozi wa jiji la Dar es Salaam ‘kuusafisha mji’ kwa kuwaondoa
barabarani na mitaani watu wote mafukara na wasio na uwezo mkubwa wa kipato.
Hawa wote wanakusanywa kwa mamia kila siku na kurundikwa Segerea kwa shtaka moja
tu linaloitwa “kesi ya kubughudhi abiria.” Uwe umekamatwa unakojoa kichochoroni,
unauza maji ya Uhai barabarani,machinga wa bidhaa,mpiga debe,unayemsubiri jamaa
yako pembeni mwa barabara au kituo cha mabasi Ubungo, uwe ni mama lishe, ni
‘dada poa’ n.k,ukishashindwa kuwakatia elfu kumi au elfu tano jamaa hao wanaoitwa askari wa
jiji au walinzi shirikishi, ujue wewe tayari unakwenda Segerea kwa kesi ileile
inayoitwa ya ‘kubugudhi abiria’. Wakati huohuo bidhaa zako zote
zinakwenda,masufuria na wali wa akina mama lishe unapelekwa kunusuru familia za
wasafisha jiji hao,simu na pesa yoyote uliyonayo mfukoni inakwenda;yaani ni
kiama! Jamani, waheshimiwa wabunge na madiwani wa jiji la Dar es Salaam hususani
wa CHADEMA chukueni hatua za haraka.
Mzee kikwete upo hapo? Unakumbuka
ahadi zako za hotuba yako ya kwanza bungeni Dodoma na wakati ulipomaliza ziara
yako ya magereza ya Keko na Segerea mwaka 2007? Achana na hayo yote,sasa njoo
gerezani upate picha ‘live’.
Nikiwa kwenye selo yangu,kwa bahati
nzuri niliruhusiwa kuletewa magazeti na kusikiliza redio . Siku moja wakati
nasikiliza kipindi cha Bunge, Naibu waziri wa mambo ya ndani akijibu hoja za
wabunge kuhusiana na hotuba ya bajeti yao iliyokuwa imewasilishwa na bosi wake
Dr.Nchimbi, nikamsikia akizungumzia swala hilo la upekuzi wa wafungwa na
mahabusu kwa utaratibu unaoonekana kumdhalilisha binadamu. Naibu waziri anasema
tatizo hilo lipo lakini kutokana na ufinyu wa bajeti hawawezi kununua vifaa vya
kisasa vya kufanyia upekuzi. Akasema kutokana na hali hiyo,wataendelea kutumia njia hizohizo za ‘ubunifu’ mpaka hapo
serikali ya CCM itakapokusanya mapato yanayokidhi bajeti inayoweza kuvinunua
vifaa hivyo.
Wakati wa kupitisha mafungu,jamaa
wakapitisha pesa ya kununua chai,vitumbua,maji ya kunywa,ziara za
viongozi,ununuzi wa magari,semina,warsha,mafunzo ,motisha n.k. Nikajiuliza,hayo
mambo ndiyo kipaumbele kweli hata kuliko kuyanunulia magereza mashine mojamoja za kufanyia upekuzi? Taasisi
mbalimbali za haki za binaadamu ni kweli zinafanya kazi nzuri kwenye mitandao
,uitishaji semina,uandikaji ripoti nyingi nzuri zinazotumwa kwa wafadhili ili
michuzi izidi kutoka n.k. lakini nasema haitoshi. Tembeleeni magerezani msiishie
kwa bwana Jela , ombeni kutembelea maeneo yote na kuongea na wafungwa . Kwa njia
hiyo mtaboresha kazi yenu kwa uzuri zaidi.
4: SALAAM TOKA MAHABUSU, POLISI NA
GEREZANI.
Mwenyekiti Mbowe alipokuja gerezani
Segerea kunitembelea akiwa na Mkurugenzi wa mambo ya Bunge na Halmashauri Bwana
John Mrema alinipa kazi ya kukijenga chama humo humo ndani gerezani . Nitakua
namkosea adabu nisipo fanya mrejesho wa kazi yake. Na kwa kuwa mengi ya yale
niliyoyafanya na kuelezwa na wadau wangu yanatuhusu sisi wote kama viongozi wa
CHADEMA, wanachama na hata wanachama watarajiwa, sio vibaya nikiyaweka
hadharani. Ya Mbowe kama Mbowe nitamuwasilishia yeye mwenyewe kwa muda
muafaka.
Wafungwa, mahabusu, baadhi ya
watumishi wa gerezani, mapolisi na wengineo wanatoa salamu nyingi sana. Wengi
wanaipongeza kazi inayofanywa na CHADEMA ndani na nje ya bunge. Wanasema karibu
wote ni CHADEMA japo wengi hawana kadi. Ili upokelewe vyema gerezani lazima uwe
‘vidole viwili’ ukijitia ‘ukada’ utalijua gereza. Wanasema kamwe wabunge wa
CHADEMA msitiwe woga na tambo za wabunge wa CCM ndani ya bunge kwa kujiona wako
wengi wakifikiria huo wingi upo hata nje ya mjengo. Wanasema katika hilo
‘wamebugi meen!!’. Nje ya Bunge CHADEMA mna mashabiki na wafuasi nyomi!!
Yaonekana kwa hivi sasa Bunge ni uwanja wa nyumbani anaoutumia CCM kimchezo na
ninyi CHADEMA uwanja wenu uko huku uraiani kwa umma.
Wanasema vitendo vya dada Makinda na
mwenzie Job Ndugai wameshavipigia hesabu. Mwisho wao hauko mbali , ninyi kazi
yenu ni kukaza buti bila kulegeza. Wamenituma niwaambie, maana mjumbe huwa
hauwawi!, eti CHADEMA nje ya Bunge tusiendelee kupoteza muda kuwahubiria watu
ufisadi, wizi, manyanyaso ya vyombo vya dola vya serikali ya CCM, kushindwa
uongozi kwa serikali nzima ya CCM, umaskini mizengwe ya CCM katika kuandikwa kwa
katiba mpya n.k. Wanasema yote hayo
wameshayaweka kichwani na wanajionea wao wenyewe kama waathirika namba moja
wanatambua fika kwamba wamo ndani ya gereza kwa sababu ya mfumo uliosababishwa
na kutengenezwa na CCM.
Wanasema katiba halisi ya watanzania
itaandikwa baada ya CHADEMA kuingia ikulu kwani CCM ni mizengwe mitupu.CCM
hawajaanza leo, kumbukeni yaliyompata Jaji Kisanga na Tume yake walipoambiwa na
Mkapa kwamba wamewasilisha taarifa ya mambo ambayo hakuwatuma. Wanasegerea wanasema elekezeni nguvu zote kwa kipindi
hiki kilichobaki kabla ya chaguzi za 2014 za serikali za mitaa na ule mkuu wa
2015 kuwapanga wapiga kura kiuchaguzi .Lipigwe jaramba na kuwekwa mpango
mahususi utakaowezesha kila aitwaye mtanzania mwenye umri wa kupiga kura apate
uhalali wa kupiga kura. Uwekwe mfumo wa kubanana kuhakikisha watu wanajipatia
vitambulisho vya uraia wanatunza shahada zao au vitambulisho na wanakwenda
kupiga kura. Wanaamini kwa hali ilivyo hivi sasa, ni binadamu ‘asiye majaliwa’
au wale wachache wasiojaa kiganjani waitwao ‘CCM maslahi’ watakaothubutu
kuelekeza kura zao kwenye rangi ya kijani- mchicha, kisamvu!
Wamo baadhi ya wafungwa na mahabusu
walionieleza kwamba walikua CCM kufa mtu na walishiriki kwenye hujuma mbalimbali
na hata kuiba kura, lakini hivi sasa wamekoma kwani wametumika kama karai na
kisha kutelekezwa nje ya jumba walilosaidia kulijenga na ndio maaana wanaozea
jela. Baadhi ya mbinu walizokua wakizitumia kutuibia kura wamenieleza na
nimetoka nazo kibindoni.
Wamenituma niwaeleze, kwa kipindi
kilichobaki, ‘chonde! Chonde! acheni kugombana, kurumbana na kufukuzana. Tumieni
kipindi hiki kujenga mshikamano utakaowezesha kukisuka kikosi cha ‘Real Madrid’
au ‘Manchester United’ ya siasa za Tanzania ili uchaguzi ujao CCM walazwe
chali-mwanguko wa kifo cha mende! Wanasema CCM ni wepesi kama nyama ya maini,
wakibanwa kwenye kumi na nane hawana ujanja
wataachia tu , tatu bila!!!
Wameniambia hivi sasa CHADEMA ni chama kikubwa
chenye uwezo wa kubuni njia mbalimbali mbadala zinazoweza kutumika kuwadhibiti
viongozi wowote au wanachama wanaodiriki
kukivuruga chama makusudi au kukihujumu badala ya kuchukua hatua za
kuwafukuza.
Wanampongeza na kumpa heko Mwenyekiti
wa chama kwa umahiri na ubunifu wake uliokifanya chama kikue na kupanuka kwa
haraka. Kwa lugha zao wanasema Mbowe ni jembe na ni kichwa,anafanya kazi nzuri
ya kutengeneza timu kwa lengo la kushinda mechi. Wanamshauri ajitahidi kuona
namna ya kuumudu mchezo ulioko mbele yetu 2014 na 2015. Iangaliwe karata
zitachangwaje? Wanasema ni vyema tukajifunze namna mchezo wa siasa za Kenya
ulivyochezwa dakika za lala salama za uchaguzi wao. Wanatambua na kupongeza
namna CHADEMA ilivyomuunga mkono Kamarade Odinga na muungano wake wa ACCORD,
lakini kwa msingi wa kujifunza mbinu za kuusaka ushindi , tuangalie na kujifunza
namna Kenyatta alivyoubadili mchezo. Kwanza kwa kumudu kuunda chama kipya na
kukijengea mtandao ndani ya muda mfupi. Pili alivyoweza kuwavuta na kuwashawishi
waliokuwa mahasimu wake walio muhimu (kama vile Ruto) ambao bila ya kuwa nao
asingeweza kufua dafu kwa Odinga. Tatu , namna Kenyatta alivyocheza mchezo wa
kisiasa kwa kuzingatia na kutumia kanuni isemayo ‘siasa hazina rafiki wala adui
wa kudumu’ bali ni kuangalia nani anawezesha kupenya vikwazo ili kuwezesha
kufika salama ninakokwenda (kwa maana ya kuingia Ikulu). Ukishaingia ndani ya
mjengo mambo mengine ni akili kichwani, utajua unachemsha vipi kichwa lakini
muhimu kuliko yote si tayari umo ndani na unachezea ndani? Wanamuomba Mbowe
azidi kuzamisha akilli na kuupanga mchezo kwa “formation” ileile ya Kenyatta,
lakini kwa kuongezea na mbinu nyingine zinazozingatia mazingira yanayotunzunguka
KICHADEMA.
5: NIMEKUTANA NA SHEIKH
PONDA
Milima huwa haikutani lakini binadamu
wanakutana. Ndivyo sakata la ugaidi lilivyonifikisha gereza la Segerea na huko
nikajikuta nawekwa selo moja na ‘mjukuu wangu’ Issa Ponda mtoto kutoka Kigoma.
Issa Ponda ni kiumbe wa mwenyezi Mungu wa aina ya pekee. Kwa nchi za wenzetu
zilizoendelea mtu mithiri ya Ponda si mtu wa kuchukulia mzaa kama ninaouona
ukichezwa hapa kwetu. Ni mtu ambaye fikra zake, ubunifu alionao kichwani na
katika vitendo, hulka zake, nasaha zake, ushawishi wake, ujengaji hoja zake,
uchaji wa Mungu wake, uswalihina wake na vingine vingi ni watu wachache sana
unaoweza kukutana nao wakiwa navyo vyote kwa mpigo.
Ponda tofauti na namna mfumo
unavyomchukulia, ni mtu ambaye angetumika vyema kwa kusikilizwa sehemu kubwa ya
mawazo yake na yakafanyiwa kazi ipasavyo, nina uhakika mambo mengi tunayoyaona
yana mitafaruku ya kidini yasingelikuwepo. Tatizo wakubwa wanamuangalia kwa
taswira ya upande mmoja ya kumuona ‘mkorofi, mchochezi’. Sijui na ndio maana
nauliza, hivi ni mamlaka gani ya juu na yenye kauli ndani ya nchi hii imewahi
kukaa na Ponda kwa karibu katika misingi ya kuheshimiana kwa dhati na
kusikilizana ili kujua ana mawazo na mitizamo gani kwa masuala mbalimbali
yaliyolalamikiwa na baadhi ya waislamu walio wengi?
Nimeishi naye zaidi ya siku 60 selo
moja kwa masaa 24 karibu kila siku na masaa mengi tukiwa wawili tu, mimi na
yeye. Ni mdadisi wa kupenda kujua, na ukisha mwelewesha ni mwepesi wa kuelewa na
kujenga fikra mpya. Hivyohivyo siyo mchoyo wa kuyabania maarifa aliyonayo na
elimu kubwa ya kidini aliyobahatika kuipata.
Alinielewesha kuwa kwenye dini ya
kiislamu mtu anapokuwa amefikia kiwango cha kuitwa U-Ustadhi kwa lugha ya haraka
inayoeleweka na wengi ni sawa na U-profesa.Hakika Sheikh Ponda ni
‘profesa’.
Nilipata fursa ya kujadiliana naye
pia mambo ya msingi yanayolikabili hivi sasa Taifa letu. Moja wapo ni nguvu
nyingi zisizo na sababu zinazotumiwa na polisi kushughulika na watu kama sisi
ambao hata rungu hatuna. Nguvu kubwa inayotumika ya kumpeleka Ponda au Lwakatare
mahakamani ili kesi itajwe tu na kurudi Segerea kulala ni sawa na kumlipa
daktari wa muhimbili mishahara mizuri ya miezi miwili. Magari nane na mapikipiki
kujazwa mafuta,ving’ora barabarani,askari polisi zaidi ya hamsini kuvunja
shughuli nyinginezo kwa siku nzima, barabara kufungwa na mengine kuzuiwa wakati
wa kupita n.k Mikwara yote hiyo ya nini?
Mfungwa mmoja aliyesoma kwa kiwango fulani alipoletwa kulala kwenye selo yetu na
kuikuta mada hiyo, alichangia hivi, “kawaida ya mtu yeyote anayelazimisha
aonekane mbele ya wakubwa zake kwamba anafanya kazi ni lazima atengeneze
mazingira yanayomfanya aonekane kweli anafanya kazi”. Kisha kasema hivi “nyie
waheshimiwa ili wale waliowafungulia tuhuma za ugaidi na uchochezi lazima watoe
taswira ya nje kwa umma kuonesha kuwa ninyi ni watu hatari sana na mkipewa
upenyo wowote mnaweza kusababisha maafa makubwa sana wakati wowote kwa taifa.
Kwa ufupi wanataka umma uwahukumu kinadharia kwamba mnahusika na tuhuma
mlizoshtakiwa nazo hata kama mahakama haijazipitia tuhuma zenyewe kuona zina
uzito gani.”
Nilimuelewa vizuri sana na
kukubaliana na huyo mfungwa maana vyombo vyetu hivi vya dola wakati mwingine vinapenda kutumia
nguvu nyingi sana katika jambo dogo sana kwa sababu tu za kuridhishana na
makundi fulani au kulinda nafasi zao za kazi ambazo hawazimudu.
Jambo jingine lililoangukia katika
mijadala yetu ni hii migogoro ya makundi ya kijamii na hata mauaji na maumizano
yanayojitokeza mara kwa mara. Sheikh Ponda alitoa changamoto moja muhimu ambayo
naona ina mashiko sana.
Alisema hivi; huko uswazi (mitaani
wanakoishi watu wengi kwa kubanana) ambako nyumba moja wanapanga na kuishi zaidi
ya watu hamsini, mchanganyiko wa waislamu kwa wakristo, mbona hakuna ugomvi?
Mbona akina mama humo ndani waislamu kwa wakristo wanaachiana watoto kwenda
sokoni? Mbona wanaazimana vijiko na masufuria? Mbona wanapeana mboga bila
kuulizana? Ponda akatumbukiza na utani pia kuwa “mbona humu selo ukileta chakula
alichopika mama Frank siulizi na wala wewe chakula anachoniletea mama Mariam
naona unabugia tu bila maswali yoyote?
Na mimi nikamwambia mbona ukiamka saa
tisa usiku ukaanza swala zako za sunna mpaka alfajiri wakati wa ‘Azanna’ na
kisha swala zote tano za ‘faradhi’ za siku nzima na lakhai zake mbilimbili humu
humu ndani ya selo havijaingiliana na ibada zangu za ‘Tumwabudu Mungu wetu?’
Selo yetu ndio msikiti wetu na ndilo kanisa letu. Haya mambo chanzo na chimbuko
lake ni nini? Hayawezi kuwa yanatengenezwa na kundi maalum la watu kwa malengo
maalum?
Swali hili la mwisho likanikumbusha
somo moja tulilowahi kufundishwa kipindi fulani nilipokwenda Ujerumani kwa
mafunzo ya ‘Strategic Planning’. Katika kipengele kimojawapo cha mafunzo hayo
nakumbuka kuna kitu mwalimu alikiita ‘Power Winning and Maintaining Strategy’,
kwa tafsiri nyepesi ‘mkakati wa kuupata utawala na kuulinda’.
Katika mkakati huo nakumbuka
alitwambia, kuna wakati watawala fulani wanapoelemewa na mambo au jambo wakakosa
majibu mbele ya watawaliwa wanaotaka kujua kulikoni ili kuzima mambo hayo aidha
ni kutumia nguvu na fursa zilizopo kumshughulikia kinara mmoja anayeonekana
kimbelembele kuhoji.
Mkisha mziba mdomo kwa njia zozote
zinazowezekana walio nyuma yake wataufyata tu! Njia nyingine ni kuibua au
kufanya jambo fulani kubwa bila kujulikana linaloweza kusaidia kuwahamisha watu
kifikra toka jambo jingine lililopo ambalo ni hatarishi zaidi
kiutawala.
Njia nyingine ni ile iliyotumika
tangu ukoloni ya ‘watawanye uwatawale’ (Divide and rule policy). Ukiwapa nafasi
au fursa watawaliwa wakakaa, wakapanga wakaelewana na nyie mpompo tu
mkiwaangalia, jua siku watakapozua ajenda ya kushughulika na wewe, ujue
umekwenda. Dawa ni kuwafanya siku zote wasielewane kwa kuwagonganisha vichwa
wenyewe kwa wenyewe tena kwa mambo madogo yasiyo hitaji gharama kubwa na nguvu
nyingi. Tulijadiliana sana na kwa urefu na Sheikh Ponda juu ya mambo haya lakini
hatukupata jibu la mwisho na kwa bahati mbaya au nzuri Mungu akawa amezisikia
dua zake na sala zake za masaa zaidi ya 18 kila siku akawa amechomolewa Segerea
na kuniachia Sello No. 3. Najua Mungu atatukutanisha tena Inshallah! Ila, isiwe
tena Segerea au Keko ili tuhitimishe mada hiyo.
Siku moja kabla ya kusomewa hukumu
yake na Hakimu Nongwa (9/5/2013) tulijadili sana hukumu yake kwamba inaweza kuwa
ya mwelekeo gani na maamuzi yapi. Panga pangua ilishindikana kueleweka mambo
yatakuwaje kutokana na mazingira yaliyokuwa yakiizunguka kesi yenyewe. Mawakili
wake walikuwa wameifanya kazi yao vyema bila kubakiza punje ya shaka. Lililokuwa
likimpa faraja zaidi na kesi yake ni kusikia kwamba huyo hakimu ni mama mlokole,
ameokoka. Hiyo ilikua ikimpa moyo sana kwamba atahukumiwa na kupewa haki yake
sawa na lile lililozungumzwa na kuwasilishwa mbele ya hakimu
Nongwa.
Nilimuuliza endapo hukumu itamuweka
katika mazingira ya kumkata makali yake ya kazi ya utetezi anayoifanya na wakati huohuo upande wa pili
wa ‘system’ ukamtaka aanze kutoa ‘Ushirikiano’ atafanyaje? Sheikh Ponda
aliniambia kuwa haki huwa hainunuliwi wala kuombwa bali hudaiwa. Alisema atakuwa
tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote yule anayezungumzia utoaji na upatakanaji
haki.Na akasema mdomo na nafsi vilivyodhamiria kuzungumzia na kuitafuta haki
huwa havifungiki kwani vikifungika hata hiyo amani haiwezi kuwepo.
Nikiwa ndani ya selo nilimsikia
Sheikh Ponda akimwaga mistari yake redioni baada ya kuhukumiwa. Kwa mara
nyingine nikazidi kumuaminia Sheikh Ponda kwamba ni mmojawapo ya watu wachache
tulio nao hivi sasa nchini wanaoweza kutembea na kuishi ndani ya maneno
yao.
Lipo jambo moja muhimu ambalo tulikubaliana na
Sheikh Ponda tulijadili na kulifanyia kazi kwa nia ya kuwanusuru watu wanaosota
jela bila sababu endapo tungeliachiwa na kuwa huru uraiani. Namtafuta kwenye
simu hayuko ‘reachable’. Nikishampata tukashauriana na likaonekana
linatekelezeka, nitalitoa hadharani.
6: USHAURI WANGU MDOGO KWA VIONGOZI WETU WA
DINI.
Mimi ni mtu mdogo sana na muumini wa
kawaida ndani ya dhehebu la KKKT. Lakini natambua kanisa ni waumini na wajibu
mkubwa wa kila muumini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kama kanisa la Mungu
linavyoelekezwa kupitia maandiko matakatifu ya Biblia. Wajibu mmojawapo sisi
kama waumini ni kuonyana ( Ebr. 10:24 – 25).
Nawaombeni viongozi wetu wa dini zote
wakristo kwa waislamu mtimize wajibu wenu mliokabidhiwa na Mungu, Imeandikwa kwa
dini zote kwamba kila mmoja bila kujali wadhifa wake atahukumiwa sawa na matendo
yake.
Nawaomba simamieni na kuuzungumza
ukweli(hata kama ni mchungu) mbele ya
watawala na hata watawala watarajiwa.Ninyi mmepewa mamlaka na Mungu ya kuonya,
kukemea, kuelekeza na kubariki na ndio maana watawala wote wanawaogopa na
kuwaheshimu. Wengine huenda ninyi bila
ya kuwatambua hutafuta njia za kujikomba kwenu ili wakipate
wanachokitafuta.Yasemeni wazi na kuyahoji hata yale machache yanayoonekana au
kusikika pasipo kificho.
Muulizeni Mheshimiwa Rais huyo waziri
wake anayezungumzwa kila siku kwamba mchana kweupe alisema anao maadui zake
wawili ambao ni waandishi wa habari na angewashughulikia, Rais analisemaje hilo?
Maadam ni ninyi, nina uhakika Mheshimiwa Rais atajibu na atachukua hatua
stahiki.
Binafsi nawaombeni kwa heshima na
taadhima muache kuwa vuguvugu (si moto si baridi-Ufunuo wa Yohana 3:15-16)
Baadhi yenu acheni kuogopa vivuli vyenu kwa maana ya kuhofia kunyimwa upendeleo
au misaada ya serikali (i.e misamaha ya kodi) na baadhi kuutumia mwanya huo
vibaya. Kama maandiko yanavyosema JIKANENI WENYEWE.
Lazima mtambue hawa jamaa wakati
mwingine huenda wanaitumia fursa hiyo kama chambo cha kuwanasia pindi wanapokua
wana taarifa zenu zote za fursa ya misamaha iliyotumika vibaya. “Mnapaswa
kushuhudiwa mema na watu walio nje…” (1 Tim 3:2-9)
Binafsi nawaomba msiwalee wala kuwabeba wale wote wenye dhamira chafu na
nia mbaya ya kutaka kuyatumia madhehebu yenu kukidhi matakwa binafsi kwani
wanachafua taswira zenu nzuri za madhehebu yenu mbele ya waumini wenu na umma
kwa ujumla.
Lakini zaidi ya yote ni imani yangu mimi binafsi kwamba madhehebu yenu ni
makubwa na yana mtandao mkubwa na wenye nguvu ndani na hata nje ya nchi.Kama
inawezekana tumieni mtandao wenu
kuisaidia serikali ambayo vyombo vyake vinaelekea kushindwa kuwabaini wahalifu
wachache wanaoelekea kuchafua na kuivuruga amani tuliyoizoea ndani ya nchi yetu.
Kwa bahati nzuri nimesoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba IGP Mwema
amezishauri taasisi za kidini kuanzisha ‘ulinzi shirikishi ndani ya misikiti na
makanisa’. Kama mambo serikali ya CCM imeyafikisha hapo, tumieni fursa hiyo
kuziomba taasisi makini mnazozifikia nje na ndani ya nchi.
7: MTIZAMO WANGU WA MBELE BAADA YA
SAKATA LA UGAIDI.
Mimi kama mimi na wakati huohuo Mkurugenzi wa ulinzi na Usalama wa
CHADEMA, kanuni yangu ya maisha ya kila siku huwa ni kutoangalia yale yaliyokwisha kuniumiza
bali ni kuangalia yanayoweza kuniumiza kuanzia leo na kwenda mbele.
Ushauri wangu wa namna gani twende
katika kukilinda chama kwa ujumla wake nitawasilisha mbele ya mamlaka na vyombo
husika vya Chama.Lakini rahi kwa wanachama wa CHADEMA na wapenda mabadiliko ya
kweli wote nchini, ni kulichukua jukumu la kuzilinda harakati hizi zinazoendelea
kama jukumu letu wote na kila mmoja kujiona anahusika na anaguswa. Chukua hatua
kuyadhibiti yale unayoweza palepale ulipo na yanayokushinda toa taarifa au
tafuta msaada kwa mtandao wa chama chetu ambao hivi sasa unaendelea
kujikita maeneo yote nchini.Asiye na
Uongozi wowote ndani ya chama wala kadi lakini anajisikia kwenye nafsi kuipenda
na kutaka kuitumikia CHADEMA, naomba achukue cheo cha u-volunteer na aingie
kazini kuanzia dakika hii na sisi tutaitambua na kuienzi kazi yake.
Kwa viongozi wangu wakuu na wale wote waliopewa dhamana ya kukisimamia na
kukiongoza chama katika ngazi na nyadhifa zozote, Sioni njia ya kutuvusha na
kutufikisha haraka tunakokwenda zaidi ya kuziendesha kazi zetu kwa falsafa ya USIMAMIZI LAZIMISHI (Lwakatare Theory).
Ni kheri ya fedheha kuliko lawama. Tujitahidi kuyafanyia tafsiri ya kutekelezeka
mambo yote tunayoazimia au kuyapanga kufanyika. Kwa njia hiyo nina uhakika
rasilimali zetu tulizonazo (fedha kidogo watu wengi) zitaweza kutuvusha na
kuyashinda mapambano yaliyo mbele yetu.
Kukaa kwangu mahabusu siku 92 kumenipa fursa ya kuyatafakari mambo mengi
kwa kina yanayonizunguka.Nimeamua NIFUNGUKE. Kufunguka kwangu ni pamoja na
kujitokeza hadharani kwenye mitandao ya kijamii kama hivi sasa nilivyoamua
kufanya jambo ambalo nilikuwa nalikwepa kutokana na watu wengi kutumia vibaya
fursa hii ambayo binadamu ameigundua.
Nilipojiunga CHADEMA, nilimuuliza mwenyekiti
angependa niifanyie nini CHADEMA kama sehemu ya mchango wangu katika harakati za
kutafuta ukombozi zinazoendelea.Aliniambia kama naweza nitumie uzoefu mdogo
niliokuwa nao kuanzia CUF wa kutengeneza mfumo wa ulinzi na usalama wa chama.
Mimi sijawahi kusomea upolisi, ushushushu wala uanajeshi labda jeshi la kujenga
Taifa mwaka 1982 Makutopora JKT Operesheni wajibu kwa mwaka mmoja. Lakini pia
japo kidogo ujumbe wangu wa muda mrefu ndani ya kamati ya ulinzi na usalama ya
CUF-Taifa, nao unaweza kuwa ulinisaidia kunitoa tongotongo kwa kiasi Fulani.
Nikiwa gerezani Segerea nilimshangaa sana ‘bwana mdogo’ Julius Mtatiro-Naibu
Katibu mkuu wa CUF alipozungumza kwenye vyombo vya habari kuwa ;”Lwakatare akiwa
CUF hatukumfundisha ugaidi.” Sikumuelewa hayo maneno alikuwa na maana gani na
alitumwa na nani. Kwanza sijui kipindi hicho nikiwa CUF yeye alikuwa wapi na
sidhani kama kwa wakati huo alifikiria hata kujiunga na hiyo CUF.Awaulize CUF
‘Original’ kama wapo, Lwakatare alikuwa ni nani ndani ya CUF.
Hata siku moja haitatokea nibeze
uzoefu na msingi wa kisiasa nilioujenga ndani ya akili zangu na nafsi yangu
kutoka CUF. CUF iliniweka katika ramani ya kisiasa ninayoitumia kutamba hadi leo
hii. CUF ilinijengea nguzo moja kubwa iliyonipaisha kisiasa na inayoendelea
kunisaidia katika kazi niliyokabidhiwa CHADEMA ya ulinzi wa chama hadi leo
ambayo ni UJASIRI WA KUJITOA KWA NAFSI
YANGU NA KWA AKILI ZANGU ZOTE KUIPIGANIA NA KUITAFUTA HAKI BILA KUCHOKA NA
KUTOKUBALI DHULUMA NA UONEVU. ‘HAKI
HUWA HULETEWI KWENYE KISAHANI CHA KIKOMBE CHA CHAI, HAKI HUDAIWA NA
KUTAFUTWA.’
Ukisha kuwa na nguzo hiyo, ni silaha tosha inayoweza kumsaidia mtu yeyote
Yule kuyaongoza au kushiriki ipasavyo katika harakati za kimapambano. Ndio maana
leo hii, wapo wanajeshi, mapolisi, usalama wa Taifa wengi mno ambao serikali ya
CCM imewadhulumu na kuwanyanyasa isivyo kawaida lakini kwa sababu ya kukosa
nguzo hiyo niliyoisema hawathubutu kujitokeza hadharani. Ganzi la CCM la
kuwafanya wawe waoga au wasijitambue limewakolea kwelikweli, hawathubutu
kufurukuta.
Wachache wanaojaribu na kuthubutu
kujitokeza wanapenda wafanye hivyo kwa kutokea mafichoni. Binafsi nawapongeza
angalau hata kwa hilo maana najua ipo siku ambayo haiko mbali, ngoma
itakapokolea watajitokeza hadharani kucheza.
Kitendo hiki cha kuvishwa tuhuma za ugaidi na kikosi cha Mwigulu na CCM
wenzake kilitukatisha sana ‘stimu’ ya kazi nyingi tulizokuwa bado tukizipanga.
Kwa wahaya wanasema, “Bampeya ntakamazile…”kwa maana ya kukatishiwa safari kabla ya kufika mwisho wa safari.
Makamanda tukaze buti, tushirikiane kwa dhati tusonge mbele mpaka kieleweke,
neema inakuja.
Afya yangu nikiwa gerezani imeathirika kidogo na kunilazimisha kufanya
vipimo ambavyo wataalam wamenieleza vinampunguzia mtu maisha yake ya kuishi.
Siliogopi hilo najua tunaye Mungu, hata nikiondoka mimi kesho makamanda wengine
wanaendelea na kazi na kusonga mbele.
Nikiwa gerezani nimezitumia siku
zangu 92 kutengeneza andiko la toleo langu la kwanza la kitabu nilichokipa
jina;
“USHINDANI NDANI YA MFUMO
KANDAMIZI (SAFARI YANGU KISIASA HADI KUTUHUMIWA KUWA GAIDI ASIYE
GAIDI).
Nimeona ni wakati muafaka kwa baadhi
ya watu wenye nia nzuri na hata mbaya wasionijua Wilfred Lwakatare ni nani
wanijue maana nikiwa gerezani yuko mwandishi mmoja wa gazeti la TAZAMA aliandika
makala yenye mtazamo wa kubeza akiuliza, “kwani Lwakatare ni nani?” Maneno
yaleyale aliyoyatumia Waziri Steven Wassira kwa mwandishi Absalom
Kibanda.
Naamini kazi na uzoefu nilioupitia wa
uanafunzi hadi chuo kikuu, uafisa utawala na utumishi serikalini, ujasiliamali,
ukulima, ufugaji, uenyekiti wa mtaa Omukituli Kibeta, uenyekiti wa CUF na
CHADEMA mkoa, ubunge wa jimbo, ukuu wa upinzani Bungeni,uratibu mkuu wa
ushirikiano wa vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, unaibu katibu mkuu
wa CUF, ukurugenzi wa ulinzi na usalama CHADEMA, ukuu wa familia ya mke na
watoto wanne na HATIMAYE kujikuta mahabusu nikituhumiwa kuwa GAIDI ASIYE GAIDI –
sio kazi za mchezo. YATAKA MOYO.
Lakini pia nimeona si vibaya
nikaonyesha uzoefu niliopitia kisiasa kwa wengine ili pale nilipokosea basi
wengine wasitumbukie katika makosa yaleyale niliyoingia. Na kama yapo mazuri ya
kujifunza, basi wayachukue na pengine kuyaboresha zaidi ili yawe chachu ya
kuwatengenezea njia katika kufanikisha malengo yao na hasa ya harakati za
kisiasa.Kwa wale watakaohitaji toleo la kitabu hicho wasisite kuwasiliana nami
kwa kunipigia simu au kutuma ujumbe wa maandishi 0713 237869, 0758 417169, 0786
774697 au barua pepe lwaks62@hotmail.com. Kwa wale wanaotaka kunisaidia kwa
namna moja au nyingine kuhakikisha toleo hilo linatoka kwa haraka na kwa
viwango, nitawashukuru kwa mikono miwili.
8: USHAURI WANGU WA BURE KWA CCM
NA WATANZANIA KWA UJUMLA.
Waswahili husema ukishikwa,
shikamana. Maana tunakoelekea sio siri CCM wameshashikwa pabaya . CCM hawana
namna ya kuyakwepa mabadiliko ya nyakati. Kukunjwa ni kuzuri kuliko
kuvunjwa.
“If they can’t change, changes will
change them.”
Watanzania ambao bado wamesinzia tokeni usingizini. Acheni kugeuzwa
mazezeta na CCM kiasi cha kushindwa kujitambua utu wenu kama watu na ubinadamu
wenu kama binadamu wanaoishi katika Taifa huru. Waache ushamba wa kuendelea
kufikiria kwamba bila kuilamba miguu CCM hawawezi kufanikiwa katika shughuli
zao. Ukombozi wa kifikra ni mkubwa zaidi kuliko ukombozi wa kutoka
utumwani.
Wajiulize wataendelea kuishi maisha
ya kila kitu ‘deal’ na uchakachuaji mpaka lini? Hawaoni kuwa ni utumwa wa
kujitakia wenyewe? Naona hata baadhi ya
hizi kesi zinazofunguliwa ni zenye msukumo wa ‘DEAL’.
Wafanyakazi na watendaji ndani ya serikali na taasisi zake nawashauri
anzeni kubadilika na kujipanga kifikra tayari kutumika chini ya utawala wa chama
chochote.
Anzeni kujiunga na chama chenu cha
AGIP (Any Government In Power) ambacho sio lazima kisajiliwe wala kutoa
kadi.
9: SHUKRANI.
Kipindi cha kukaa kwangu gerezani
kililikua cha mtihani mkubwa kwangu ambacho kimenipa mafunzo tosha katika
maisha. Gerezani sio mahala pa kumuombea au kuombea mtu kupelekwa . Ni mahala
ambapo kwa wengine panakua chanzo cha familia kugombana, kufarakana,
kusambaratika, ndoa kuvunjika na uadui kujengeka baina ya mtu na mtu, na mengine
mengi. Baadhi nimeyashuhudia mimi mwenyewe kwa macho yangu.
Binafsi nashukuru kwa ukaribu niliopewa na familia, ndugu, jamaa,
marafiki, viongozi wa chama, wanachama na wanajela wenzangu. Ukaribu wao wa muda
wote uliifanya siku iwe fupi.Sio siri ndugu zangu, unapotembelea ndugu yako
aliyeko gerezani furaha unayomuachia mule ndani haipimiki.
Namshukuru sana mke wangu Angel Mercy kwa
kukikabili kipindi chote hicho kigumu kwa kunipa huduma, kufuatilia afya yangu,
kuiangalia na kuitunza familia iliyopo nyumbani na watoto walioko mashuleni
licha ya yeye mwenyewe kukabiliwa na masomo chuoni,Mzumbe-Mbeya.
Nawashukuru sana ndugu zangu kaka,
dada zangu, ndugu, marafiki, majirani na watoto wetu wote kwa misaada waliyonipa
kupitia kwa mke wangu lakini kubwa kuliko yote kitendo chao cha kuja kuniona
gerezani.
Nikishukuru chama, (CHADEMA) kwa
kunipigania na kunitolea misaada isiyohesabika. Kipekee nimshukuru sana Katibu
Mkuu Dr. Slaa kwa ufuatiliaji mkubwa alioufanya.
Pongezi na shukrani nyingi kwa jopo
zima la mawakili mahiri. Peter Kibatala, Tindu Lissu, Mabere Marando, Prof.
Abdallah Safari na Nyoronyo kichehere, ambao najua bado tuko pamoja katika ngwe
ya pili ya kesi ya shitaka moja ambalo bado linanikabili na huenda na mazagazaga
mengine yanayoweza kujitokeza.
Nivishukuru kwa namna ya pekee vyombo
vya habari vilivyofuatilia na vinavyoendelea kufuatilia sakata zima la kesi
yangu na kuifahamisha jamii kujua kinachoendelea.
Niwape pole na shukrani nyingi wale
wote waliofika gerezani na kushindwa kuniona kutokana na idadi kuwa kubwa kuliko
idadi ya watu walioruhusiwa kuniona.
Kipekee nimshukuru sana Baba Mchungaji wa
usharika wetu wa King’ong’o Kimara na mke wake. Mr & Mrs Rev Joseph Kyaka
walionitembelea na kunijengea moyo wa imani, matumaini na faraja.
Niwashukuru wote waliokuwa pamoja
nami kifikra na kimaombi na ninasema kwa maombi yenu, yote yamewezekana. Mungu
anasikiliza maombi na haachi kujibu.
Nimuombe Mungu azidi kututangulia na kutupa ujasiri wa kukabiliana na
adui na kumshinda shetani huku tukidumu katika imani.
IN GOD I TRUST.
IMEANDALIWA NA:
WILFRED MUGANYIZI
LWAKATARE
MKURUGENZI WA ULINZI NA USALAMA
CHADEMA.
No comments:
Post a Comment