Taarifa
iliyopo ni kwamba mnamo tarehe 21 Mei 2013 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya
Umoja wa Afrika (AU) Addis Ababa nchini Ethiopia, ulipofika wasaa wa Mh. Rais Jakaya M.
Kikwete kusema aliyokuwa nayo, alitumia fursa hiyo kuishauri serikali ya Rwanda ikiongozwa na Raisi Paul Kagame juu ya
hali ya amani nchini Congo.
Alimsihi ya kwamba ili hali ya amani irejee, hana budi kufanya mazungumzo na
kundi la FDLR, waasi wa Kinyarwanda walioko Congo.
Ushauri huu
ulikuwa kama cheche kwenye kichaka maana kilichofuata hapo ni kama ambavyo
tumeshuhudia serikali ya Rwanda
ikionyesha kugadhabishwa kwa hali ya juu kutokana na ushauri huo.
Kabla
sijarejea kwenye mada kuu iliyonifanya niandike, ningependa kuchambua ushauri
huu kimtizamo binafsi na kwa kutuma utashi (common
sense) ambao kila mwanadamu
amejaliwa. Mtu anapokushauri jambo, na zaidi zaidi awe ni mshirika wako (katika
hali hii wahusika ni maraisi wa nchi jirani), unaweza kuuchukua ushauri huo na
kumshukuru, pengine hata kumdadisi juu ya namna ya kuufanyia kazi kwa maono na
maoni yake. Pili, kama ni ushauri
usioshabihiana na mtizamo wako au utashi wako juu ya mambo, utaukataa. Ni jambo
la nadra sana kukuta mtu anakataa ushauri kwa
ukali na lugha ngumu kama aliyotumia Mh. Kagame labda awe na ukosefu wa staha
(kitu ambacho siamini raisi wa Rwanda
kapungukiwa kwacho). Hivyo basi inanifanya niamini kukaripiana huku ni hatua ya
mwisho kabisa ya tatizo ikiashiria kuwa kumekuwa na misuguano ya chini kwa
chini ambayo kwa namna moja au nyingine haikufika kwenye vyombo vya habari.
Hata hivyo, naepuka kujihusisha na utabiri (speculations).
Nini basi
alichokisema Raisi Paul Kagame? Alipokuwa akihutubia wahitimu wa mafunzo ya
kijeshi katika chuo kilichopo Musanze, mnamo tarehe 10, Juni 2013, (nitanukuu
na kutafsiri yale muhimu kwa mujibu wa video ipatikanayo mtandaoni (youtube)
iitwayo (President Kagame on Kikwete’s statement) alisema
“…nilisikia
kuna baadhi ya watu walikuwa na mambo ya kusema kuhusu Rwanda kufanya
mazungumzo, kujadiliana na wauaji wa watu wetu…watu wanaizungumzia FDLR
kirahisi rahisi hivyo…na wanajua wanazungumzia makaburi haya ya watu wetu, na
kwamba wale waliofanya hivi (waliofanya kitendo cha mauaji)…tuna deni kwao.
Hata hivyo, awali sikusema kitu juu ya hili, kutokana na mosi, kuchukizwa nalo,
pili nilifikiri ni upuuzi mtupu, tatu, labda ilitokana na umbumbumbu, nne…kama
ni tatizo la kimlengo, (na nadhani ndio tatizo kuu) basi tatizo hilo ni bora
likabaki na wenye nalo…lakini tutapata siku nyingine ya kulikabili hilo (tatizo)…”
Ikafuata
hotuba ya Mh. Raisi Kikwete mwishoni mwa mwezi Julai ambayo ilisheheni mambo
kadha wa kadha likiwemo la uhusiano baina ya Rwanda
na Tanzania.
Nitanukuu yale machache nyenye manufaa katika andiko langu hili;
“…napenda
kuwahakikishia watanzania wenzangu na ndugu zangu wa Rwanda kuwa mimi na
serikali ninayoiongoza tunapenda kuwa na ushirikiano mzuri…mimi na serikali
ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya vitendo vibaya dhidi ya serikali ya
Rwanda au nchi yoyote jirani au nchi yoyote duniani…napenda kuwahakikishia
ndugu zetu wa Rwanda kuwa kwa upande wetu hakuna kilicho badilika wala kilicho
pungua katika uhusiano na ushirikiano..
…kwa
upande wangu binafsi, sijasema lolote kuhusu Rwanda,
pamoja na maneno mengi kutoka Rwanda
na viongozi wake, pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli kutoka kwenye
vinywa vya viongozi wa Rwanda
dhidi yangu…sio kwamba sisikii, wala si kwamba siambiwi yanayosemwa au sijui
kusema, au sina la kusema, la hasha! Sijafanya hivyo kwasababu sioni faida
yake…”
Kwa
mtizamo wa karibu wa hotuba hizi mbili; yaani ile ya Mh. Kagame na ile ya Mh.
Kikwete zina ujumbe (tone) tofauti. Wakati ile ya awali ikionekana kutoka kwa mtu
mwenye gadhabu, ya mwisho inaonekana ikitaka kusawazisha hali (atmosphere) ilo tengenezwa na ile hotuba
ya mwanzo.
Shida inakuja
pale vyombo vya habari vinapozinasa hotuba hizi mbili na kuamua kuleta muktadha
viutakavyo vyenyewe sijui kwa manufaa ya nani.
Gazeti la Mwananchi, Agosti 3 lilibeba kichwa cha
habari kisemacho “Kikwete amvaa Kagame, amshangaa kwa lugha za matusi na kejeli.”
Jambo la kujiuliza hapa ni je? kulikuwa na “kuvaana” kupi katika hotuba ya Mh.
Raisi, kama sio kutia chumvi kwenye kidonda?
Muandishi wa makala husika alimnukuu raisi Kagame kwa kusema,
“…nilinyamaza
kimya kwasababu sikupenda kusikiliza ushauri kuhusu FDLR, kwa sababu nafikiri
ni upuuzi ulioambatana na ujinga. Hatuwezi kuacha maisha yetu kama
Wanyarwanda tunavyoishi sasa. Ushauri wa kikwete ni sawa na kucheza na makaburi
ya watu wengi ambao ni ndugu zetu”
Kwa mtu makini
ni rahisi kugundua kuwa nukuu hii imeongezwa chumvi hasa ikizingatiwa kwamba
Rais Kagame hakumtaja Raisi Kikwete katika hotuba ile.
Hata yale
magazeti ambayo huitwa ya “udaku” (sijui kwanini) kama
vile Uwazi
yakajitosa. Katika toleo lake la tarehe 6 agosti, lilibeba kichwa cha habari “choko
choki za Rwanda,
Kagame kukiona”. Pia liliambatana na picha za vifaa mbali mbali vya
kijeshi (bila shaka kuashiria nguvu ya kivita ya Tanzania). Je? Katika hotuba ya Mh.
Raisi, alilenga ujumbe ufikishwe kwa mantiki hii? Ni kweli kwamba raisi
alilenga kutoa onyo kwamba tuko tayari kwa vita na jirani zetu?
Makala
nyingine iliyoandikwa katika gazeti la Mwananchi
la tarehe 21 Agosti ilibeba kichwa kisemacho “Kagame kujenga nchi miaka,
kuibomoa dakika”. Kwa juu juu, kichwa hiki cha habari hakina madhara
yoyote, ila mpaka pale utapo ingia na kusoma undani wake. Moja ya aya ilisema;
“Chuki
za Kagame dhidi ya kikwete zimeibuka pale Tanzania ilipoamua kupeleka majeshi
yake DRC kwa mapendekezo ya UN kwa ajili ya kulinda amani katika kifungu cha
saba, kinacho ruhusu kujibu mashambulizi pale askari wa kulinda amani wanapo
shambuliwa.”
Sijui na sidhani kama muandishi wa makala husika hapo anao
ushahidi wa kutosha juu ya hilo alilopenda kutuaminisha ya kwamba kisa cha
uhusiano wa nchi hizi mbili kuharibika ni kutokana na sababu hiyo ya askari wa
Tanzania kuingia nchini Congo .
Mwandishi wa makala hiyo pia anajitahidi kuihusisha serikali
ya Rwanda na uwepo wa
kikundi cha M23 kule Congo
pale anaposema;
“…lakini uhusiano huu umeanza kuingia
dosari pale Tanzania
ilipoamua kuingilia mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) pale
ilipokitaka kikundi cha M23 kiondoke katika nchi hiyo ya Afrika ya kati.”
Huu ni uandishi unaotia doa taaluma ya uandishi wa habari
maana hakuna vyanzo vyovyote vya habari vinavyo nukuliwa ili kuthibitisha madai
haya. Na hata kama vyanzo vingenukuliwa, hadithi ilipaswa kufunika pande zote
mbili (yaani ile ya wanaodai Rwanda
inahusika na M23, na ile inayopinga).
Kwa upande mwingine, vyombo vya habari vya nchini Rwanda
navyo havikuwa nyuma.
Mara baada ya kutoka kwa makala tajwa hapo juu ya gazeti la Mwananchi,
gazeti la The New times la Rwanda la Tarehe
27 Agosti, liliandika hivi; “war mongers in Tanzania
media: Rwanda supports
peace, not war” na kwa tafsiri isiyo rasmi ni “wachochezi wa vita
katika vyombo vya habari Tanzania:
Rwanda
inapenda amani na sio vita.” Andiko hili lilikuwa jibu la andiko la gazeti la Mwananchi
nililojadili awali. Tofauti ni kwamba wakati mwandishi wetu akichochea
mtafaruku, mwandishi wa Kinyarwanda ambaye ni Stephen Ruhanamilindi
alitofautiana na hali hiyo.
Hata hivyo, gazeti hilo hilo la Tarehe 9 Agosti lilichapisha
toleo lenye kichwa cha habari kisemacho “Govt reassures Tanzanians as Kikwete kicks
out Rwandans”, likiwa na maana “serikali yawapa uhakika watanzania
(waishio Rwanda) huku Kikwete akiwafukuza Wanyarwanda.” Tatizo la kichwa hiki
cha habari, kinamfanya mtu aamini kwamba Raisi Kikwete kawafukuza Wanyarwanda
kibaguzi ilhali si kweli. Katika hotuba yake niliyonukuu hapo awali, alipata
kutoa agizo kwamba wale wote waliohamia nchini Tanzania isivyo halali, basi
wahalalishe ukaazi wao au la warudi makwao. Kama
wanyarwanda ambao tumewasikia wakilalamika baadae kuwa wamefukuzwa baada ya
kuishi nchini miaka yote walikuwa na uhalali wa kuendelea kuishi, hapakuwa na
ugumu wowote wa kuhalalisha ukaazi huo.
Gazeti la The News of Rwanda la tarehe 19 Agosti,
nalo lilibebelea kichwa cha habari kilichosema Tanzania president Kikwete
“married to Habyarimana Cousin”, kikimaanisha Raisi wa Tanzania Kikwete
kamuoa binamu yake Habyarimana. Ndani yake kuna aya isemayo;
“New
details obtained by News of Rwanda may give insight into why Tanzania’s
president Jakaya Kikwete came out as the sole global leader symphatheic to
Rwandan FDLR rebels based in DR Congo jungles since 1994.
According
to secret US State Departement cables published by whistle blowing site
Wikileaks, President Kikwete’s wife fondly known in Tanzania as Mama Salma
Kikwete is a cousin of former Rwandan Leader Habyarimana.”
Tafsiri yake ni
kwamba “Taarifa mpya zilizoifikia News of
Rwanda (gazeti) zinaweza kutoa mwangaza wa kwanini raisi wa Tanzania amekuwa mtu pekee kuwahi kuwatetea
waasi wa Kinyarwanda, FDLR walioko nchini Congo tangu 1994. Kwa mujibu wa
taarifa za siri kutoka wizara za marekani zilizovujishwa na mtandao wa
wikileaks zimeeleza kuwa mke wa raisi wa Tanzania maarufu kama Mama Salma ni binamu yake kiongozi wa
zamani wa Rwanda.”
Juvenal Habyarimana alikuwa ni Raisi wa Rwanda mwenye
asili ya ki Hutu aliyeuawa mwaka 1994 kwa ndege aliyokuwa akisafiria
kulipuliwa, jambo lililochochea vita vya kimbali baina ya wa Tutsi na wa Hutu.
Kuna mambo kadha wa kadha ya kushangaza juu ya aya hizo
kutoka kwa mwandishi huyo aitwaye Gahiji. Mosi,
kuna tatizo gani la Mama Kikwete kuwa binamu yake Habyarimana. Kama
kweli Wanyarwanda ni watu waliosameheana (reconciled kama wasemyavyo) kutokana
na tofauti zao za kikabila zilipopelekea takriban watu 800,000 zaidi zaidi wa
asili ya kitusi kuuawa na wahutu, iweje kuwa ndugu wa mhutu marehemu
Habyarimana liwe jambo la kushitua sana?
Pili, kulikuwa kuna utetezi gani wa wahutu (FDLR) kutokana
na tamko la Raisi kikwete la kuwataka wakae faragha na kurejesha amani ya
mashariki ya kati?
Tatu, je? Kulikuwa na uhitaji gani wa kuanza kufukua historia
ya mke wa Raisi ambaye kwa mujibu wa Wanyarwanda, amewaghafirisha sana? Huu sio uchochezi?
Kwenye matatizo baina ya pande mbili, ni busara kuzidi fukua matatizo au
kutafuta suluhu ili kuleta hali ya amani?
Nikihitimisha uandishi wa andiko hili, ningependa kuweka
bayana kwamba baadhi ya vyombo vya habari
vya nchi hizi mbili (Rwanda
na Tanzania)
havijatenda kwa kutumia busara na weledi ili kuzuia hali mbaya kuwa mbaya
zaidi. Ni vyombo hivi ndivyo vimekuwa na mchango mkubwa katika kuwaaminisha
Wanyarwanda na Watanzania kwamba kuna tatizo kubwa ilhali hakuna tatizo au kama lipo basi ni dogo na kwamba taarifa za kusawazisha
hali ya taharuki na sintofahamu ndizo zingepewa kipaumbele. Badala yake, sijui
ni kwa uchu wa kufanya biashara, au kuchochea uhasama, vyombo hivyo vimekuwa
vikichochea moto kwenye tofauti iliyojitokeza.
Wakati suala hili linatarajiwa kumalizika kidiplomasia siku
za usoni, nitoe rai kwamba vyombo vya habari vina nguvu kubwa sana ya kujenga
na kuharibu/kubomoa kwa maana ya kuweza kuuaminisha umma kuwa nyeupe ni nyeusi
na nyeusi ni nyeupe wakati sivyo na matokeo yake kupelekea kuwepo kwa jamii
iliyogubikwa na uvunjifu wa amani na manung’uniko. Hivyo basi, penye fursa ya
kurejesha amani kwenye mgogoro, media
zitumike kufanya hivyo na siyo kuchochea tofauti kupitia machapisho.
No comments:
Post a Comment