Kwa kauli hiyo, Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upunzani Bungeni, amefuta rasmi minong’ono ya muda mrefu kwamba anakusudia kuwania tena urais baada ya kufanya hivyo mwaka 2005.
Akizungumza na wananchi wa Karatu kwenye Uwanja wa mpira wa Karatu baada ya kumaliza kikao chake na viongozi wa Karatu, Mbowe alisema kwa sasa amejielekeza kupanga na kutekeleza mikakati kuhakikisha CHADEMA inaingia Ikulu mwaka 2015 na kuhakikisha anasimamia kupata viongozi bora wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha upinzani.
Mbali na kusimamia upatikanaji wa mgombea bora wa urais, Mbowe alisema pia kazi yake kubwa itakuwa kuhakikisha anasimamia upatikanaji wa wagombea bora wa nafasi zote za uongozi kuanzia ngazi ya serikali za vijiji, vitongoji, madiwani, wabunge na urais.
“Kuna taarifa za upotoshaji zinaenezwa kuwa mimi na Dk. Slaa tuna ugomvi wa kuwania urais. Jambo hili sio kweli hata kidogo, mimi sitawania urais mwaka 2015 na Dk. Slaa nafanya naye kazi kwa kuheshimiana na maelewano ya hali ya juu kwani tumekuwa wote kwa muda mrefu sasa,” alisema Mbowe.
Alitamba kuwa CHADEMA itaingia Ikulu mwaka 2015 na itachukua majimbo mengi ya uchaguzi na kutolea mfano wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini kwamba kati ya majimbo 22 yaliyopo, chama hicho kina uhakika wa kushinda 15.
Kuhusu mgogoro wa Karatu uliokipasua chama hicho katika makundi, Mbowe alisema umemalizika baada ya kikao chake na viongozi hao kwa siku mbili.
Katika kuonesha kwamba viongozi hao wamemaliza tofauti zao, Mbowe aliwapandisha jukwaani viongozi wote na kushikana mikono kama ishara ya kutakiana amani.
Mwaka 2000, Mbowe alikuwa Mbunge wa Hai, lakini ilipofika mwaka 2005, chama kilimwomba kuwania urais, hivyo aliacha kuwania ubunge licha ya wananchi wa Hai kumtaka asiache.
Source....jamii forum
No comments:
Post a Comment