ZIARA ya Rais wa Marekani, Barack Obama hapanchini, ‘imeivua nguo’ Serikali ya Tanzania, baadaya vyombo vya habari vya kimataifa kutoa tuhuma
nzito za vitendo vya kikatili vinavyodaiwa kufanywa na vyombo vya dola dhidi ya raia.
Hatua hiyo inayodaiwa kujaribu kufichwa kwa nguvu kubwa na baadhi ya watendaji wa serikali,
imekuja kufuatia baadhi ya vyombo vya habari mashuhuri nchini Marekani, kuibua upya tuhuma
za utekaji, upigaji na uuaji wa raia, waandishi wa habari na wanaharakati nchini Tanzania.
Moja ya chombo kilichoanika uovu huo, ni gazeti kongwe na mashuhuri linaloheshimika sio tu
Marekani, bali na mataifa makubwa la New York Times, ambalo Julai 1, 2013, lilichapisha habari
isemayo ‘Matukio ya udhalimu yaongezeka Tanzania, Kisiwa cha Amani Afrika’.
Habari hizo zilizoandikwa na mwandishi maarufu wa habari za uchunguzi duniani, Nicholas Kulish
zimeeleza tukio la kusikitisha la kutekwa nyara na kuumizwa vibaya kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari nchini, Dk. Stephen Ulimboka, kama mojaya tukio baya ambalo linadaiwa kuwa na mkono wa serikali, ingawa Rais Jakaya Kikwete aliwahi kukanusha madai hayo.
Mwandishi huyo ameeleza namna Dk. Ulimboka alivyotekwa na kupakiwa kwa nguvu katika gari
linaloaminika kuwa la moja ya vyombo vya usalama, kupigwa kwa kikatili kwa nyaya,
kung’olewa kucha, na jinsi watesaji walivyoshauriana njia ya kumuua ikiwemo kumkanyaga na gari ama sindano ya sumu. Mwandishi huyo, amemnukuu, Dk. Ulimboka akisema namna alivyowasikia watesaji wake, wakimwambia kuwa ‘atalipa yote aliyotenda’ na
kumtaka asali na kumwomba Mungu wake, kwa sababu hataiona dunia tena.
Aidha, gazeti hilo limeieleza dunia kutekwa kwa waandishi wa habari na kuuawa kikatili kwa
mwandishi wa habari, Daud Mwangosi aliyeuawa na askari polisi akiwa kazini, katika Kijiji cha
Nyororo, mkoani Iringa, mwaka jana.
Katika kuonesha uzito wa tuhuma hizo na namna wananchi wa Marekani wanavyotaka
lishughulikiwe haraka, moja ya taasisi kubwa inayotetea waandishi wa habari duniani, yenye
makazi yake jijini New York, ilimwomba Rais Obama kumkabili Rais Kikwete watakapokutana katika ziara yake iliyomalizika jana, juu ya matukio hayo na uhuru wa vyombo vya habari.
Kadhalika, gazeti hilo limeanika matukio mawili ya mashambulizi ya mabomu yaliyofanywa jijini
Arusha kwenye Kanisa la Katoliki la Olositi na katika mkutano wa chama cha upinzani, (hawakukitaja) na kusababisha vifo vya watu saba.
Gazeti hilo pia limeeleza kwa kirefu namna shambulio la bomu la kurushwa kwa mkono
lilivyotokea katika mkutano wa CHADEMA hivi karibuni huko jijini Arusha, na shutuma
zilizotolewa na chama hicho dhidi ya Jeshi la Polisi kuhusika na kumtorosha aliyelipua bomu hilo.
Kadhalika, limenukuu msimamo wa CHADEMA wa kukataa kukabidhi kile kinachosemakana mkanda mzima’ wa tukio hilo kwa polisi, hadi pale itakapoundwa tume huru kuchunguza tukio hilo. Msimamo huu wa New York Times, wa kuichimbua Tanzania na kuyaanika maovu yake yote
unaungwa mkono pia na magazeti mengi nchini Marekani, kama vile USA Today, ambalo nalo
limechapisha habari zenye msimamo kama huo, likionesha wazi namna ziara ya Rais Obama ilivyotoa fursa ‘kumulikwa’ kikamilifu kwa matukio mabaya yaliyoikumba nchi. Inadaiwa kwamba mara baada ya waandishi hawa wa Marekani kupata taarifa kutoka kwa Wizara ya
Nje ya Marekani (State Department), juu ya ziara ya Obama hapa nchini, walianza kujipanga kufichua maovu yanayotendwa na Serikali ya Kikwete.
Vyombo hivyo, vikafichua matukio mabaya yakiwemo uvunjwaji wa haki za kibinadamu,
matukio ya matumizi ya nguvu kupita kiasi kwa upande wa polisi, kutokamilika kwa uchunguzi kwa
matukio ya kihalifu na uhasama baina wa wafuasi wa chama tawala na wale wa upinzani, Mbali na matukio hayo, vyombo hivyo, kinyume na vya hapa nchini ambavyo vimesifia ziara ya Obama,
vimejikita kuibua uozo uliopo, likiwemo pia suala la kukithiri kwa uchafu katika Jiji la Dar es Salaam.
Chombo kingine kilichoandika mabaya ya Tanzania
ni wavuti ya eTurbroNews ambayo inaandika
kuhusu masuala ya utalii. Watuti hiyo, Julai 1, 2013, iliibua habari za uchafu
uliokithiri jijini Dar es Salaam, na kulitaja kuwa
mojawapo ya majiji yanayosifika kwa uchafu
likishika nafasi ya 12 duniani. Habari hiyo imeushutumu uongozi wa jiji kwa
kuamka dakika za majeruhi kufanya usafi na
kujiuliza ilikuwaje wasubiri hadi ziara ya Obama
kufanya kazi hiyo. Aidha, habari hiyo imezungumzia kero ya kunguru
weusi, na kushauri pengine ianzishwe kampeni ya
watu kutoka nje kuja kuwawinda na
kuwaangamiza kabisa, kama mchezo wa uwindaji,
kwani sasa idadi ya kunguru hao waharibifu inazidi
milioni moja.
source-JF
No comments:
Post a Comment